HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 16 July 2018

KALIUA YATOA PIKIPIKI 12 KWA MAOFISA UGANI ILI WAENDE KWA WAKULIMA

Na Tiganya Vincent, Tabora
JUMLA ya watumishi 12 wa Kada mbalimbali wa Halmashauri ya  Wilaya ya Kaliua wakabidhiwa pikipiki zenye thamani ya milioni 29  kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma mbalimbali kwa wakulima na wananchi wanaoishi vijijini.

Akiongea kabla ya kukabidhi pikipiki hizo jana  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt. John Pima alisema kuwa lengo la utoaji pikipiki hizo ni kutaka Maofisa Ugani na Watendaji wa Kata waweze kuwafikia wakulima na wananchi mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia.

Alisema utoaji wa pikipiki hizo ni utekelezaji wa agizo la viongozi wa Kitaifa la kuwataka Maofisa Ugani kuondoka Ofisini na kwenda kwa wananchi kwa ajili ya kuwaelimisha juu kulima kilimo kilicho bora ambacho kitawawezesha kuzalisha kwa tija kwa ajili ya kuongeza kipato chao na kuwapata ziada kwa ajili ya kuuza.

Dkt. Pima alisema katika mwaka wa fedha walishatoa pikipiki 8 kwa ajili ya Maofisa Ugani Kata na Watenadaji wa Kata na wataendelea kununua pikipiki kwa kutumia mapato ya ndani hadi hapo watakapo hakikisha watumishi wa kada hiyo wanavyo vyombo vya usafiri kwa ajili ya kusaidia wananchi ikiwemo kulima kilimo bora na kusikiliza kero zao.

Alisema Halmashauri hiyo ili kuhakikisha inatekeleza agizo la viongozi imeshawasambaza Maofisa Ugani katika maeneo mbalimbali ya vijijini kwa ajili ya kuwasogeza karibu na wananchi ili watumie utaalamu wao kuwasaidia wakulima na sio kutoa maelekezo wakiwa ofisini.

Akikabidhi pikipiki Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alilipongeza Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri hiyo kwa kutekeleza haraka agizo la viongozi wa kitaifa la kuwataka watendaji kwenda kusikiliza kero za wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaonya Watumishi waliopatiwa vyombo hivyo wa usafiri kuhakikisha wanavitumia kusaidia wananchi na wakulima na sio kwa ajili ya maslahi binafsi ikiwemo kugeuza ‘boda boda’na kuongeza kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi .

Alisema baada ya watendaji hao kupata usafiri anatarajia kuona mabadiliko na mapinduzi ya kilimo katika maeneo yote ambayo Maofisa Ugani wamepatiwa pikipiki ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji kwa upande wa wakulima na kutatuliwa kero ya wananchi.

Mwanri alizitaka Halmashauri nyingine za Mkoa wa Tabora kuhakikisha nazo zinawawezesha Maofisa ugani kuanzia ngazi za vijiji hadi Kati ili wawasadie wakulima waweze kuondokana na kilimo cha kizamani ambacho hakifuati kanuni za kilimo bora kinachozalisha ziada na kumwondoa katika umaskini.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasele alisema Baraza la Madiwani wataendelea kutenga mapato yao ya ndani kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ununuzi vyombo vy usafiri kwa watendaji mbalimbali.

Alisema lengo ni kutaka kuleta mapinduzi ya kilimo Wilayani humo ili kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali kwa ajili ya kuuza ndani na nje.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akipanda pikipiki kabla ya kuzikabidhi jana kwa Watendaji wa Kata na Maofisa Ugani wa Kata mbalimbali wilayani Kaliua ili waende vijijini kutoa  huduma kwa karibu kwa wakulima na wananchi wengine.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kulia), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Haruna Kasele(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama (kushoto) wakijaribu pikipiki kabla ya kukabidhi jana Watendaji wa Kata na Maofisa Ugani wa Kata mbalimbali wilayani Kaliua ili ziwasaidie kwenda kutoa huduma kwa karibu kwa wakulima na wananchi wengine. Picha na Tiganya Vincent.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad