HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 9 May 2018

TPDC yawanoa viongozi wa dini kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendeleza utaratibu wake wa kutoa elimu zaidi juu ya sekta ya gesi asilia na mafuta kwa wadau mbalimbali safari hii ikiwa ni kwa viongozi wa dini kutoka Mkoa wa Lindi. Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba, Meneja Mawasiliano wa TPDC, Bi. Marie Msellemu alisema “huu ni muendelezo wa mikakati ya Shirika katika kujenga uelewa na mahusiano bora na wadau ambapo leo hii tupo na viongozi wa dini kutoka katika vijiji na mitaa linapopita bomba la gesi kwa Mkoa wa Lindi”. 

Bi. Msellemu alieleza kwamba, TPDC akiwa kama shirika la mafuta la Taifa linalo jukumu sio tu la kuzalisha na kusambaza gesi asilia bali pia kuhakikisha elimu sahihi juu ya manufaa na faida za miradi ya gesi asilia inapatikana kwa wadau wote. Bi. Msellemu alifafanua kwamba, TPDC iliona ni vema kuwajengea uelewa zaidi viongozi wa dini kwani wao ni nguzo muhimu katika jamii na pia ni watu wenye ushawishi mkubwa hivyo kuelewa kwao juu ya maendeleo ya sekta ya gesi asilia na mafuta kutasaidia kusambaza uelewa zaidi kwa waumini wao. 

Ziara ya viongozi wa dini kutoka Mkoani Lindi haikuishia katika kutembelea kiwanda cha kuchaka gesi asilia pekee bali pia walipata fursa ya kusikiliza mada kuhusiana na maendeleo katika mkondo wa juu na mkondo wa chini katika sekta ya mafuta na gesi asilia. Mada hizi zilitolewa na wataalamu kutoka TPDC ambapo, Ndg. Shaidu Nuru, Mjilojia kutoka TPDC alitoa mada kuhusu maendeleo katika mkondo wa juu na kugusia hali ya utafiti nchini kwa sasa na maendeleo katika mradi mkubwa wa LNG. Akitoa mada hiyo, Ndg. Shaidu alisema “ utafiti wa mafuta na gesi asilia nchini ni zoezi endelevu ambalo limepelekea ugunduzi mkubwa wa shehena ya gesi asilia (futi za ujazo 57.83 trilioni) katika nchi kavu na kina kirefu cha bahari”. 

Kwa upande wake Mha. Aristides Katto, Afisa Utafiti kutoka idara ya mkondo wa chini alifafanua maendeleo na mikakati mbalimbali ya TPDC katika kusambaza gesi asilia pamoja na kugusia faida na manufaa ya rasilimali hiyo. Akitoa mada hiyo Mha. Katto alisema “ TPDC iko katika maandalizi ya utaratibu wa namna ya kushirikiana na sekta binafsi katika zoezi la kusambaza gesi asilia kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam ambapo inatarajiwa kwamba utaratibu huu utarahisisha usambazaji kwani sekta binafsi ina nafasi ya kipekee katika kukuza uchumi wa Taifa”. 

Akizungumza kwa niaba ya viongozi walioshiriki katika ziara na semina hiyo,  Abdallah Hokororo aliishukuru sana TPDC kwa kuandaa zoezi hilo na kusema “kiukweli kwangu mimi ziara hii imekuwa ni ya manufaa sana kwani huko mitaani kuna wanaosema mambo mengi kuhusu gesi ikiwa hawana taarifa kamili lakini leo hii nimepata nafasi ya kufahamu vema kuhusu sekta hii kutoka kwa wenyewe TPDC na kwa hakika nitaenda kuwa balozi mwema huko niendako”.  TPDC ndio msimamizi na mshiriki katika shughuli za utafiti, uendelezaji, usambazaji na uuzaji wa gesi asilia hapa nchini, shughuli aifanyayo kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati. Sheria ya Petroli ya 2015 (PA,2015) imeipa TPDC hadhi ya kuwa kampuni ya Mafuta ya Taifa na pia kuipa hakio za kipekee katika shughuli za ukusanyaji, usambazaji na uuzaji wa gesi asilia hapa nchini. 
 Viongozi wa dini kutoka mkoani Lindi wakitembelea kiwanda cha kuchakata gesi asilia, Madimba-Mtwara
Maalamu kutoka TPDC, Godbless Swagarya akifafanua jambo kwa viongozi wa dini walipotembelea kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba, Mtwara. 
Sehemu ya viongozi wa dini kutoka Lindi wakiwa katika ziara ya kutembelea kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba, Mtwara. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad