HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 9 May 2018

Michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA kutumika kuibua vipaji vya wanamichezo nchini

Na Genofeva Matemu – WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka walimu wa michezo nchini kutumia michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA kuibua vipaji kupitia hazina ya vijana wadogo waliopo katika shule za msingi na sekondari wenye uwezo mkubwa katika michezo mbalimbali.
Rai hiyo ameitoa Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na wadau wa sekta ya michezo kujadili namna ambavyo michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA itakavyoendesha mwaka huu ambapo michezo hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Juni mwaka huu Jijini Mwanza.
“Tumedhamira kuibua vipaji kuanzia ngazi ya shule za msingi ili tuweze kuliweka taifa katika taswira ya michezo kwani michezo ni sayansi inayohitaji mazoesi yanayoweza kuisaidia jamii kuwa na afya bora na hata kuweza kuitangaza nchi katika mataifa mengine kupitia michezo mbalimbali” amesema Mhe. Mwakyembe.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewataka wadau wa michezo nchini kujitokeza kwa wingi kuchangia ili kufanikisha michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA na kuifanya michezo hiyo kuwa agenda kubwa hapa nchini katika kuendeleza michezo na kuinua vipaji vya michezo mbalimbali.
Aidha Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dkt. Yahya Msigwa amesema kuwa Michezo ni kila kitu katika jamii kwani michezo ni ajira, michezo ni siasa, michezo ni kinga dhidi ya ukimwi na kinga dhidi ya ujambazi kwa vijana, michezo ni biashara, michezo ni utamaduni na pia michezo haina mipaka kati ya nchi na nchi.
“Kama tunataka kweli mabadiliko chanya katika michezo ni lazima tuanze na watoto waliopo katika shule za msingi na sekondari ili tuweze kuwajengea uwezo na kuimarisha michezo kwani huko ndiko chimbuko la michezo linapoanzia” amesema Dkt. Msigwa.
Naye mwakilishi kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Maganga Japhet amesema kuwa wadau wa michezo nchini wanapaswa kusaidiana kwa pamoja na serikali katika kuboresha mkakati huu wa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji kupitia michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwani kwa kufanya hivyo kutalifanya taifa kuwa na wachezaji wazuri walioandaliwa kuanzia ngazi ya chini. 
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi na wadau kuelekea mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamed Kiganja
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akifafanua jambo wakati wa kikao cha maandalizi na wadau kuelekea mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Elimu Bw. Tixon Nzunda
 Baadhi ya wadau wa sekta ya michezo wakifuatilia hoja wakati wa kikao cha Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kuelekea mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA Jijini Dar es Salaam
 Mwakilishi kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Maganga Japhet akichangia mada wakati wa kikao cha Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kuelekea mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA  Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kulia waliokaa) pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(wapili kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa michezo walioshiriki katika kikao cha maandalizi kuelekea mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA Jijini Dar es Salaam. Picha na Genofeva Matemu - WHUSM

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad