HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 9, 2018

Balozi Seif awataka wananchi kuchangia damu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa kila Mwananchi mwenye sifa za uchangiaji damu kuanzia umri wa Miaka 18 hadi 65 uzito wa Kilogram 50 ajitokeze kujitolea kuchangia damu ili kuiepusha Jamii kukumbwa na upungufu wa damu salama Nchini ambao wakati mwengine huleta athari.

Alisema upungufu mkubwa wa Damu uliojitokeza Mwaka uliopita hasa katika Kipindi Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa Taarifa za uchangiaji Damu Salama katika Maabara za Mahospitali Zanzibar ulipelekea kwenda kuomba Damu Tanzania Bara.

Akizungumza katika Bonaza la Uchangiaji Damu Salama lililoandaliwa na Mkoa wa Kusini Unguja na kufanyika Dunga Wilaya ya Kati Balozi Seif Ali Iddi alisema kwa mujibu wa Takwimu zilizopo inaonyesha kwamba mahitaji halisi ni chupa 1,250 kwa Mwezi kwa matumizi ya kawaida Unguja na Pemba.

Balozi Seif alisema shughuli za uchangiaji wa damu salama  humgusa kila mwana jamii  hivyo ipo faida kubwa inayopatikana licha ya kuokoa maisha ya walio wengi ambao hupatwa na matatizo ya kiafya lakini pia humrahisishia Mtu kuweza kupima maradhi mbali mbali bure bila ya gharama sambamba na kuelewa afya yake.

Aliwaasa Wananchi kutambua umuhimu wa kuokoa maisha yao wenyewe wakiwa kama wana Jamii hasa wanapoelekea katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani  ambao wengi hushindwa kuchangia Damu kwa wakati  pale wanapokuwa na mgonjwa anayehitaji huduma hiyo kwa haraka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kitendo hicho hupelekea usumbufu mkubwa kwa Madaktari na wahudumu wa Afya na hatimae mgonjwa anayekumbwa na kadhia hiyo wakati mwengine huishia kupoteza maisha.

Balozi Seif  alielezea matumaini yake kwamba uwezo wa kukusanya Kiwango cha chupa 1,250 kwa Mwezi upo kwa vile Taifa limebarikiwa kuwa na Wananchi Wazalendo wenye nguvu na Afya Bora ambao wanaweza kuchangia bila kipingamizi kwa kuokoa Taifa.

Alifahamisha kuwa Damu hiyo inaweza kutumika kwa kuwasaidia walengwa katika Makundi mbali mbali wakiwemo Wajawazito, Wahanga wa ajali mbali mbali, Wagonjwa wa upasuaji pamoja na Watoto wadogo.

Aliupongeza Uongozi wa Mkoa Kusini Unguja kwa jitihada ulizoonyesha na hatimae kufanikisha zoezi hilo la kuwahamasisha Wananchi wa Makundi mbali mbali kwa ajili ya kuchangia Damu na kukidhi mahitaji ya Maabara  za Hospitali zilizopo Nchini.

“ Hongereni sana Mkoa Kusini Unguja kwa jitihada mlizozionyesha na hatimae kujaza pengo liliopo. Matumaini yangu ni kwamba baada ya zoezi hilo Maabara zetu zitasheheni Damu hasa kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na ikiwezekana mpaka Mfunguo Mosi”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliyashauri maeneo mengine ndani ya nje ya Nchi kuendeleza desturi hiyo ya uchangiaji Damu Salama kila inapoonekana ulazima wa kufanya hivyo baada ya kushaurina na Kitengo husika.

Alisema ni vyema Desturi hiyo pia ikaelekezwa katika kuwatia moyo na hamasa wale ambao bado hawajashiriki katika mazoezi na Mabonaza hayo ili waweze kuungana na Wananchi wengine katika matukio hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii yote.

Akitoa Taarifa ya zoezi hilo Afisa uhamasishaji wa kuchangia Damu kutoka Jumuiya ya Wachangiaji Damu Zanzibar Bwana Bakari Mabarawa alisema hilo ni Bonaza la Tano kati ya Kumi yanayoendelea kufanyika katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Magarawa alisema kufuatia hatua za Wananchi kuhamasika yapo matumaini makubwa ya kuvuka malengo ya matarajio katika Kampeni ya kuhamasisha Jamii kupenda kuchangia Damu salama.

Mhamasishaji huyo wa uchangiaji Damu wa Jumuiya ya Wachangiaji Damu alifahamisha kwamba Kituo cha Huduma za Damu Salama bado kimekabiliwa na changamoto ya upungufu wa Watendaji tokea kilipoanzishwa mnamo Mwaka 2008 ambao huathiri zoezi la utoaji Damu pale wanapobahatika kutoa huduma kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya Wananchi waliohamasika.

Alisema zipo juhudi zilizochukuliwa na Kituo hicho za kuwafunza Vijana 15 kwa takriban Miaka Miwili sasa na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwapatia Ajira Vijana hao Wazalendo ili kuondosha kabisa changamoto hiyo.

Naye Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Hamad Rashid Mohamed  akimkaribisha Mgeni Rasmi kuzungumza na Wananchi hao kwenye Bonaza hilo alisema hilo ni jambo muhimu kwa Uhai na Afya ya Wanaadamu.

Mh. Hamad alisema Watu  wote ni wahitajiwa wa kutoa na kupewa Damu Salama jambo ambalo ni wajibu kulisimamia ipasavyo sambamba na kulitekeleza kwa nguvu zao zote.

Waziri wa Afya alizipongeza Wilaya mbali mbali Nchini kwa kusimamia Mabonaza ya Uhamasishaji uchangiaji Damu salama ambazo zimetekeleza wajibu wao bila ya kuwa na Kasma ya kazi hiyo muhimu kwa Ustawi wa Jamii.

Waziri Hamad aliihakikishia Jamii kwamba Wizara hiyo itajenga mazingira ya uwepo wa Vituo vya Maabara kwa ajili ya kupatikana kwa huduma za Damu salama kwenye Hospitali za Wilaya zote Unguja na Pemba ili kuondosha usumbufu wa kufuata huduma hiyo masafa marefu zilipo Hospitali Kubwa.

Alisema Mpango huo unaotarajiwa kuanza miezi ya hivi karibuni ni utaratibu unaozingatia kuteremshwa kwa madaraka Mikoani na Wilayani kupitia Mfumo ulioanzishwa wa Ugatuzi.

Bonaza hilo la uchangiaji Damu salama lililoambatana na upimaji wa Maradhi ya Macho, Moyo pamoja na Sukari limeshirikisha Vikosi mbali mbali vya Ulinzi na Usalama, Wananchi wa kawaida pamoja na Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.
 Wataalamu wa Kitengo cha Huduma  za Damu Salama wakianza zoezi la kuwapima Wananchi waliojitokeza kuchangia Damu kwenye Bonaza la Uchangiaji Damu la Mkoa Kusini Unguja lililofanyika Wilaya ya Kati Dunga.
Wananchi mbali mbali wakipata ushauri nasaha kutoka kwa Wataalamu wa Kitengo cha Huduma  za Damu Salama kabla ya kuchangia Damu kwenye Bonaza la Uchangiaji Damu la Mkoa Kusini Unguja.
Afisa uhamasishaji wa kuchangia Damu kutoka Jumuiya ya Wachangiaji Damu Zanzibar Bwana Bakari Mabarawa aliyenyanyua  mikono akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya Kampeni ya Uchangiaji Damu Salama unavyofanywa katika maeneo mbali mbali Nchini.
Mmoja wa Mchangiaji Damu aliyejitokeza kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bwana Sabri Yussuf Ali akichangia Damu kwenye Bonaza la Uchangiaji Damu la Mkoa Kusini Unguja lililofanyika Wilaya ya Kati Dunga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na wananchi wakati wa kichangia Damu kwenye Bonaza la Uchangiaji Damu la Mkoa Kusini Unguja lililofanyika Wilaya ya Kati Dunga.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad