HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 11 May 2018

MAPATO YA UTALII YAONGEZEKA KUTOKA DOLA BIL. 1.7 HADI KUFIKIA DOLA BIL. 2.2

Na Octavian Kimario
Mapato yanayotokana na utalii yameongezela kutoka Dola za Marekani Bil. 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 2.2 mwaka 2017 ambapo ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi A. Kigwangalla alipokuwa akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018.

" Wote tunaelewa ya kuwa Utalii ni moja wapo ya sekta zinazokua kwa kasi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kupunguza umasikini wa kipato. Sekta ya utalii inachangia takriban asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni (foreign exchange earnings)," alisema Dkt. Kigwangalla.

Aidha amesema, mafanikio ya Sekta ya Utalii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na juhudi za Serikali  kutekeleza Sera hiyo kwa ushirikiano na wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za utalii, utangazaji katika masoko mbalimbali ya utalii duniani na mazingira bora ya uwekezaji.

Dkt. Kigwangalla ametaja masuala ambayo yametiliwa mkazo katika  Sera hiyo kuwa ni pamoja na Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wote wa utalii katika kuhifadhi rasilimali za utalii, kuendeleza rasilimali watu, kuimairisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa,  kuimarisha mnyororo wa thamani katika mazao ya utalii pamoja na kuongeza wigo wa mazao ya utalii (kama vile kuendeleza utalii wa fukwe na utalii wa mikutano).

Vile vile kuweka mkazo katika kutangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii kimataifa,  kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji,  pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani na kuendelea kusimamia viwango vya ubora wa huduma za malazi nchini.

" Mtakubaliana nami kuwa, leo tunayo kazi kubwa iliyopo mbele yetu, hivyo ni vema kuweka mawazo yetu kwa pamoja katika kipindi cha masaa machache yajayo na kuibuka na maboresho kwa ajili ya rasimu hii ya Sera kwa mustakabali wa sekta ya Utalii nchini," alifafanua Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema Sera ya Taifa ya Utalii iliyopo sasa ilifanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 18 iliyopita.

Amesema, katika kutambua hilo, Wizara iliona ni muhimu kupitia upya Sera hii ili kuhakikisha kuwa ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini, unaenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani yakiwamo mabadiliko ya teknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira.

"Aidha, kwa kuzingatia kuwa msingi mkuu wa kuandaa Sera yeyote ni kuwashirikisha wadau ambao ndio watekelezaji wa Sera hiyo,mapitio ya Sera hii, yameshirikisha wadau wote muhimutangu hatua za awali," alisema Meja Jenerali Gaudence Milanzi.

Warsha hiyo  imejumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi ambao kwa namna moja au nyingine huguswa au hushiriki katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mej. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza na Washiriki wa warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Warsha hiyo leo Jijini Dodoma.
  Waziri wa Maliaasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Washiriki wa warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 wakati alipofungua Warsha hiyo leo Jijini Dodoma.
  Washiriki wa warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 wakimsikiliza Waziri wa Maliaasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (hayupo pichani) alipofungua Warsha hiyo leo Jijini Dodoma.
Waziri wa Maliaasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara, Wadau wa Sekta ya Utalii na Washiriki wa Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 wakati alipofungua Warsha hiyo leo Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad