Na Bashir Yakub.
Ni muhimu kujua tofauti ya kisheria ya maneno ubatili na ubatilifu kabla ya kujua lolote kuhusu hadhi/nafasi ya kisheria ya ndoa pasi na tendo la ndoa. Ujuvi wa maneno ubatili na ubatilifu ndio utakaopelekea kufahamika vyema kwa haya makala. Kisheria kuna tofauti kati ya ubatili na ubatilifu.
1.TOFAUTI YA KISHERIA KATI YA UBATILI NA UBATILIFU.
( a ) UBATILI.
Maana ya ubatili kisheria ni kuwa jambo hilo haliruhusiwi kabisa. Halitakiwi kutendwa kwa namna yoyote ile . Kwa lugha ya kitaalam matendo haya huitwa “VOID ACTS”. Ni matendo haramu kabisa. Kwa mfano kwenye ndoa matendo haramu ni pamoja na mtu kutangaza ndoa na mtoto wake wa kuzaa, au mtu na mzazi wake, au kutangaza ndoa ya jinsia moja au kutangaza ndoa na mtu mwenye umri mdogo. Kwa namna yoyote matendo haya ni batili( void), haramu na hayaruhusiwi kwa namna yoyote.
( b ) UBATILIFU.
Maana ya ubatilifu kisheria ni kuwa tendo linakuwa si halali wala si haramu isipokuwa ili liwe halali au haramu litategemea uamuzi wa upande mmoja kati ya pande mbili zilizokubaliana. Upande mmoja unaweza kuamua jambo liwe halali au liwe haramu , nitatoa mfano.
Mtu akikuuzia gari ambalo liko tofauti na ulivyokuwa umemwagiza katika mkataba wenu tendo hilo sio halali wala sio haramu/batili ila ni batilifu. Hii ina maana kuwa ukiamua kulipokea gari hilo na kulikubali hivyohivyo lilivyo basi umehalalisha tendo hilo na limekuwa halali. Ukikataa kulipokea kwakuwa linapingana na kile kilicho kwenye makubaliano basi tendo hilo la kuletewa gari lililo tofauti linakuwa haramu/batili.
Basi ifahamike kuwa katika sheria yapo matendo ambayo si halali wala si haramu. Na haya kwa kitaalam huitwa”voidable acts”. Na hicho ndicho kitakachoelezwa katika kujibu swali la nafasi ya kisheria ya mtu ambaye hawezi kutekeleza tendo la ndoa.
2. KUTOWEZA KUTEKELEZA TENDO LA NDOA.
Sheria imesema kushindwa kutekeleza tendo la ndoa”incapable of consummating”. Maana ya hili ni kushindwa kabisa kutekeleza tendo la ndoa na sio uwezo mdogo katika kutekeleza tendo la ndoa. Tofauti hii ni lazima ipambanuliwe bayana.
KUSOMA ZAIDI sheriayakub.blogspot.com
No comments:
Post a Comment