Meneja wa Mawasiliano TCRA Makao makuu Innocent Mungy akizungumza na Wanahabari kuhusu zoezi la kuzifungia Simu Bandia na zitakazobainika kutumia Namba za Usajili Bandia ifikapo June 16,2016 katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Zanzibar Ocean View mjini Zanzbar .
Baadhi ya wandishi wa Habari waliofika katika Mkutano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCTA unaohusu kuzifungia Simu Bandia ifikapo Juni 16 kwaka huu.
Naibu Mkurugenzi, masuala ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Thadayo Ringo akimuanyesha mmoja wa wandishi namna ya kuweza kuijua simu Bandia.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 03.02.2016
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imesema ifikapo June 16 mwaka huu itavifungia Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi hususan Simu na Tableti ambavyo vinatumia namba tambulishi Bandia.
Hatua hiyo ni miongoni mwa njia muhimu za kudhibiti wizi wa Simu na kuhimiza utii wa sheria nchini.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Mawasiliano Makao makuu Innocent Mungy alipokuwa akizungumza na Wanahabari kuhusu kuzifungia Simu hizo katika ukumbi wa Zanzibar Ocean View mjini Zanzbar.
Amesema kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 kinataka kuwepo kwa Mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa Vifaa vya mawasiliano na inawataka watoa huduma za mawasiliano yanayotumia vifaa vya mikononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba Tambulishi ya vifaa hivyo.
Mungy amefahamisha kuwa mfumo huo wa kielektroniki ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la Mawasiliano.
Aidha amesema kuwa vifaa vyote vya mawasiliano ambavyo Vimeibiwa, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza kufanya kazi kwenye mitandao ya mawasiliano kuanzia Juni 20.
“Mfumo huu sio mgeni kwa nchi za wenzetu hata Kenya wanatumia na tayari wameshazifungia Simu Feki kwa hiyo kabla sisi kuzifungia tunalazimika kuwaelewesha Wananchi kabla ya hiyo June 16 Mwaka huu” amesema Mungy.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Masuala ya Watumiaji wa huduma za mawasiliano TCRA Thadayo Ringo akielezea faida za huduma hiyo amesema iwapo mtu amepoteza au kuibiwa Simu ya mkononi na akatoa taarifa kwa Mtoa huduama, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote nchini.
Aidha ametoa wito kwa wananchi mara tu wanapopoteza simu zao za mkononi kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya kituo maarufu kama RB kama utibitisho wa umiliki wa simu iliyopotea.
Akizungumzia juu ya hatua za kuchukua iwapo Mtu atakuwa na simu Bandia isiyokidhi viwango amesema itamlazimu mtu anunue simu nyingine kwa gharama yake.
Akielezea namna ya kutambua namba Tambulishi Ringo amesema mtumiaji atatakiwa aandike Tarakimu *#06# kwa kutumia Simu yake ambapo kutaonekana namba ndefu na hivyo namba hizo kutakiwa azitume kwa njia ya ujumbe mfupi kwenda namba “15090” ambapo atapokea ujumbe kufahamisha uhalisia wa simu yake.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kwa sasa wapo Zanzibar kutoa elimu kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya kuwajengea uelewa wananchi kutambua iwapo Simu zao hazitumii namba tambulishi Bandia kabla ya kuzifungia ifikapo June 16 2016.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment