HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 14, 2012

MASHIRIKA YA KIMATAIFA YAMUAGA DK. ASHA-ROSE MIGIRO

 Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Ban Ki Moon akiongea katika hafla ya kumuaga Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Dk. Asha-Rose Migiro mara baara ya kumaliza muda wake.
 Dkt Asha-Rose Migiro baada ya kupokea zawadi ya maua katika hafla hiyo ya kumuaga rasmi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiwa na Dkt Asha-Rose Migiro katika hafla ya kumuaga rasmi iliyofanyika leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza muda wake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Dkt Asha-Rose Migiro akiongea katika hafla hiyo ya kumuaga rasmi

    Na  Mwandishi Maalum
Mashirika ya  Umoja wa Mataifa yanayohusika na  masuala ya  Idadi ya Watu ( UNFPA),Ugonjwa wa Ukimwi ( UNAIDS) na   Mpango wa  kupambana na Ugonjwa wa Malaria ( RBM) jana jumanne yaliandaa tafrija kamambe ya kumshukuru  na kumuaga Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro.
 Tafrija hiyo ya aina yake  na ambayo  mgeni  rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Ban Ki Moon,  akiambatana na mke wake na kuhudhuriwa pia na  wadau  mbalimbali  akiwamo Mtendaji  Mkuu wa UNDP Bi Helen Clark, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika UM,  sekta binafsi na taasisi za kiraia imefanyika hapa makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza wakati wa  tafrija hiyo, Katibu Mkuu Ban ki Moom ameleezea baadhi ya  sababu  zilizomsukuma  kumteua Dkt. Asha- Rose Migiro kuwa msaidizi wake wa karibu.
 “ Nilianza kumfahamu Asha- Rose Migiro wakati huo sote tukiwa mawaziri wa mambo ya nje  katika nchi zote. Uwezo wake na uelewa wake wa mambo ulinivutia sana, lakini nilivutiwa zaidi pale nilipofahamu kwamba aliwahi kuwa waziri anayehusika na masuala ya wanawake na watoto.

Nikajiridhisha kwamba huyu ndiye alikuwa ananifaa kuwa msaidizi wangu wa karibu” akasema Ban Ki Moon na kuufanya umati ulihohudhiria tafrija hiyo kushangilia kwa nguvu.
 Kama hiyo haitoshi, Ban Ki Moon amemuelezea Dkt. Asha- Rose Migiro kama msaidizi wake wa karibu ambaye licha ya kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa lakini ni mtu ambaye alikuwa hana makuu na wala hata siku moja hakujikweza.
“ Katika kipindi chote ambacho Migiro amekuwa msaidi wangu wa karibu, amenisaidia katika mambo mengi, ni mtu muadilifu sana, ni mtu aliyekaribu sana na watu, aliyeamsha matumaini na kuwapa tabasamu watu waliokuwa katika mazingira magumu.  Daima amekuwa mstari  wa mbele kunisaidia  na hakuna hata siku moja alipojikwenza. Na kwa sababu hii  anastahili tafrija hii” akasisitiza Ban Ki Moon.
Aidha Ban Ki Moon akamuelezea  Asha- Rose Migiro kama kiongozi ambaye daima alitoa kipaumbele  cha aina yake katika masuala ya afya ya jamii  eneo alilotumia uwezo wake wote, maarifa yake yote kama naibu katibu mkuu kupigania afya ya wanawake na watoto na watu wote walio katika mazingira magumu.
Kwa upande wao waandaaji  wa tafria hiyo na wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemuelezea  Naibu Katibu Mkuu, kama kiongozi ambaye mchango  wake umesaidia sana katika  kuihamasisha jumuiya kimataifa kuweka mkazo wa aina yake katika kushughulika afya ya jamii.
Bw. Michel Sidibe, Mkurugenzi mtendaji wa  UNAIDS yeyé alimuelezea Asha- Rose Migiro kama dada yake ambaye sifa zake zinaazia mbali.
“ Asha- Rose Migiro ni dada yangu, ni dada ambaye anasifa za kipekee, ni mwanamke wa kwanza  aliyefaulu  kwa daraja la kwanza katika sheria kutoka chuo kikuu cha dar es Salaam,  ni mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa mambo ya nje nchini Tanzania,  na ni mwanamke wa kwanza kutoka afrika kuwa naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa” akasema Bw. Sidibe kauli iliyoamsha tena makofi kutoka kwa wageni waalikwa.
Hakuishia hapo, Michel Sidibe akamuelezea Migiro kama kiongozi aliyefanya kazi  kwa karibu na  Shirika lake katika kuhakikisha kwamba  maambukizi ya  virusi vya ukimwi yalikuwa yakipungua ikiwa   ni pamoja na kupatika kwa tiba ya uhakika kwa waathirika.
“ Tunakila sababu leo hii kumshukuru kwa namna alivyoshirikiana nasi, na ingawa  unaondoka lakini tambua kwamba mchango wake utaendelea kukumbukwa na kuenziwa” akasisitiza  Bw. Michel Sidibe.
Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika la Umoja wa Maifa la  Idadi ya Watu, Dr. Babatunde Osotimehin amesema  juhudi kubwa zilizoonyeshwa na  Naibu Katibu Mkuu  katika  kushughulikia masuala ya afya ya jamii, kumefanikisha kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi  hali kadhalika vifo vya watoto wachanga chini ya miaka mitano.
“Katika kipindi  cha uongozi wako, umefanikisha sana katika kuhamasisha  jumuia ya kimataifa kuongeza  misaada yao na kutoa kupaumbele katika afya ya mama na mtoto, tunakushukuru sana kwa hili, na   Mungu aendelee kukubariki” akasema Dr. Babatunde Osotimehin.
Kwa upande wake,  Bw. Herve Verhoosel,  Mwakilishi wa  Mapango wa kupunguza Malaria, yeyé alimuelezea  Dkt. Asha-Rose Migiro kwamba chini ya  uongozi wa Ban Ki Moon, ameweza kujenga misingi bora ya  ushirikiano   na muamko   miongoni mwa wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba  kunakuwapo na uhusiano kati ya sekta za umma za zile za binafasi katika kutimiza malengo ya afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kasi ya kupunguza malaria.
 Akiwashukuru waandaji wa tafrija hiyo, Naibu Katibu Mkuu amemshukuru Katibu Mkuu Ban Ki Moon kwa kumuamini kuwa msaidizi wake wa karibu katika kipindi cha miaka mitano na nusu.
Akasema   ingawa yeyé amejituma  na kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, lakini amefanya hivyo kwa kuwa Ban Ki Moon alimuamini kwamba anaweza. Na kwamba daima ataendelea kuienzi heshima hiyo.
Akatumia fursa hiyo kumueelezea Ban Ki Moon kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba kila mtoto angalau alikuwa analala kwenye chandarua, akina mama wajawazito walikuwa hawapotezi maisha kutoka  na uzazi.
Aidha  Migiro amewashukuru kwa moyo wa dhati wasaidizi wake wa karibu  aliofanya nao kazi akiwa naibu katibu mkuu na kwamba bila wao asingefika hapo alipo, akawashukuri pia wadau mbalimbali wakiwamo mabalozi kwa ushirikiano wa hali na mali waliompatiwa muda wote wa miaka mitano na nusu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad