HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 14, 2012

MKURUGENZI WA UTALII ZANZIBAR AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utalii Zanzibar Alhalil Mirza akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali kuhusiana na safari yake ya kikazi nchini Ujarumani.Hafla iliofanyika huko ofisini kwake Amani Mjini Zanzibar.

Na Ramadhani Ali – Maelezo,Zanzibar

Shirika la ndege la Qatar, Air Qatar, linatarajia kuanza safari zake kuja Zanzibar kuleta watalii kutoka nchi mbali mbali za asia na nchi nyengine za ulaya miezi michache ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amani, baada ya kurejea kutoka kwenye maonyesho ya kimataifa ya ITB mjini Berline Ujerumani, Mkurugenzi mkuu wa shirika la utalii Zanzibar ndugu Ali Khalil Mirza amesema hatua hiyo imefikiwa kufuatia mazungumzo yaliyofanywa na ujumbe wa Zanzibar kwenye maonyesho hayo ulioongozwa na Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Abdilahi Jihadi Hassan.

Amesema kuja kwa ndege za shirika hilo kutaongeza idadi ya watalii wa daraja la juu kuitembelea Zanzibar kwa vile Qatar ni kiungo kikubwa cha watalii kutoka mataifa mbali mbali duniani kote.

Ndugu Mirza ameongeza kuwa katika ziara hiyo ya siku tano wamefanya mazungumzo na makampuni mengine ya ndege ili yaweze kufikiria uwezekano wa kuleta watalii Zanzibar likiwemo Shirika la ndege la Air Arabia na yameonyesha nia ya kutekeleza makubaliano ya mazungumzo yao kwa vitendo.

Mkurugenzi mkuu amesema hadi sasa kuna mashirika makubwa manne ya ndege na ndege ndogo nane yanayoleta watalii moja kwa moja Zanzibar na takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya watalii laki mbili wa ndani na nje wanatembelea Zanzibar kwa mwaka na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kufuatia ziara hiyo.

Amewaeleza waandishi wa habari kwamba katika maonyesho yaliyoanza tarehe saba hadi tarehe 12 mwezi huu, kampuni tisa za uuzaji misafara ya watalii Zanzibar zilizoshiriki wametiliana mikataba na kampuni za misafara ya utalii ya nchi za ulaya hatua ambayo itaimarisha utalii wa visiwa vya Zanzibar.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu kwa Zanzibar kujipanga na kuandaa utaratibu mpya wa kujitangaza zaidi nje na ndani na kuimarisha vianzio vilivyopo vya utalii na kubuni vianzio vyengine vipya ili kuweza kushindana kwani soko la utalii hivi sasa linaushindani mkubwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad