Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akiongea na Mabalozi wa Tanzania Nchi za nje waliomtembelea ofisini kwake.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliomtembelea ofisini kwake. Kuanzia kushoto Balozi Ladislaus Komba (Uganda), Balozi Shamim Nyanduga (Msumbiji), Balozi Grace Mujuma (Zambia) na Balozi James Alex Msekela (Italia).
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja leo amekutana na Mabalozi wa Tanzania nchi za nje kwa lengo la kueleza juu ya fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta za Nishati na Madini nchini.
Mabalozi hao wanaowakilisha Tanzania nchi za nje walikutana na Waziri Ngeleja ofisini kwake kwa ajili ya kupata taarifa zaidi kuhusiana na sekta za nishati na madini nchini ili waweze kuzitangaza sekta hizo nchi za nje.
Waziri Ngeleja aliwafafanulia juu ya fursa mbali mbali za kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na sheria mbalimbali za madini ambazo kwa namna zilivyo zinaweza kuwa ni chachu ya kumvutia muwekezaji.
Aliwaomba mabalozi hao wajitahidi kuhakikisha wanaitangaza Tanzania huko waendako ili kuvutia wawekezaji.
“Jamani nawaombeni sana mkaitangaze nchi yetu, hususan katika sekta za Nishati na Madini ili tupate wawekezaji wakubwa ambao watasaidia zaidi katika kuinua uchumi wa nchi yetu” Aliwaambia waziri Ngeleja.
Waziri Ngeleja aliwaeleza Mabalozi hao juu ya ugunduzi mbalimbali wa gesi nchini na kubainisha kuhusu Makampuni mbalimbali ya nchi za nje ambayo yapo nchini kwa ajili ya utafiti zaidi. Aidha, alisema utafiti zaidi unaendelea na vilevile aliwaomba mabalozi hao watangaze juu ya tafiti hizo ambazo huenda zikawavutia zaidi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania.
Naye Dokta Batilda Buriani, Balozi wa Tanzania nchini Kenya alisisitiza juu ya kuwa na mikakati ya pamoja ya kuhakikisha Tanzanite inatangazwa kuwa ni mali ya Tanzania na siyo nchi nyingine yeyote duniani. Kuhusu suala la Tanzanite, waziri Ngeleja aliwatoa hofu mabalozi hao na kuwaeleza kuwa hivi sasa kuna hati maalum ambayo itatumiwa katika madini ya Tanzanite ambayo inatambulisha ni wapi madini hayo yanatoka. (Certificate of originality)
“Kwakuwa tunawafahamu wanunuzi wakubwa wa Tanzanite, tunaendelea kuwashawishi kutokununua Tanzanite isiyokuwa na certificate of originality” alisisitiza Waziri Ngeleja
Mabalozi hao walimuahidi Waziri Ngeleja kuwa watahakikisha wanaitangaza Tanzania vizuri zaidi kuhusu sekta za Nishati na Madini kwakuwa hivi sasa wamepata uelewa mkubwa zaidi.
Akiongea kwa niaba ya mabalozi wengine, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Ladislaus Komba alisema “Tutahamasisha wawekezaji huko tuendako kwa kuwa sasa hivi tunauelewa wa kutosha juu ya sekta hizi mbili hivyo inakuwa rahisi sana kwetu kuitangaza nchi yetu”
Mabalozi waliokutana na Waziri Ngeleja ni Balozi Shamim Nyanduga (Msumbiji), Balozi James Alex Msekela (Italia), Balozi Grace Mujuma (Zambia), Balozi Ladislaus Komba (Uganda) na Balozi Batilda Buriani (Kenya).
No comments:
Post a Comment