HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 11, 2011

watakaobainiika kufanya uzembe uliosababisha kuzama kwa meli ya Spice Islanders kuchukuliwa hatua


Waziri katika Afisi ya Makamo wa pili wa Rais, 
Mhe Mohamed Aboud Mohamed

Na Salama Njani – Habari Maelezo Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainiika kufanya uzembe uliosababisha kuzama kwa meli ya Spice Islanders huko katika mkondo wa Nungwi hapo jana na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo mjini Zanzibar , Waziri katika Afisi ya Makamo wa pili wa Rais, Mhe Mohamed Aboud Mohamed amesema,kuwa kamati maalum itaundwa ili kuchunguza juu ya ajali hiyo na ikibainika kuwa uzembe umepatikana sheria itachukua mkondo wake.

Mhe Aboud amesema kuwa Serikali hivi sasa imejikita zaidi katika suala la uokoaji na kubainisha waliofariki ili watakaotambuliwa waweze familia zao kwa mazishi na wale ambao hawatotambulika Serikali inachukua jukumu la kuwazika.

Amesema kuwa uchunguzi ni kitu cha lazima ili kujua ukweli ulivyo na kama makosa yametokezea yaweze kurekebishwa na yale ambayo yakitokea kwa uzembe uliofanywa basi hatua za sheria zitachukua mkondo wake na Serikali haitosita kufanya hivyo.

Mhe Waziri amesema kuwa tatizo kubwa la wazanzibari ni muhali, na amesema ili utendaji mzuri uwepo, lazima suala hili la muhali liwekwe upande ili nchi ipige hatua za maendeleo, na ikibainika kuna watu wanafanya uzembe wa kikazi lazima hatua za kisheria zichukuliwe hapo hapo, na Serikali hii itafanya hivyo .

Akijibu swali kuhusu tatizo la usafiri na uwezekano wa Serikali kumiliki meli zake ambazo zitahakikisha kuwa na usalama zaidi amesema, ni kweli tatizo la usafiri lipo, lakini serikali kupitia mfumo wa Uchumi na biashara huru, imetoa fursa ya watu binafsi kuanzisha na kumiliki vyombo vya usafiri, ili kutoa fursa zaidi ya biashara na ukuaji wa Uchumi.

Hata hivyo amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatafakari juu ya suala hilo ili kuona vipi wanaweza kufanya vizuri katika kazi ya kuwa na meli, kwani uzoefu umeonekana kuwa bado Zanzibar haijawa na wataalamu wa kutosha kuliendesha Shirika la Meli, na Serikali kuogopa kuingia katika suala hilo kwani Mashirika mengi yamekufa.

Kuhusu Nahodha wa Meli hiyo amesema kuwa mpaka hivi sasa bado hajapatikana na haieleweki kuwa yuhai au amefariki lakini muhandisi wake yuhai na ameokoka na hivi sasa anachukuliwa Maelezo na vyombo vinavyohusika.

Akijibu juu ya suala la jina na mmiliki wa kampuni hiyo amesema kuwa mpaka sasa hawamjui mmiliki wa kampuni ya Meli hiyo,lakini atawapatia jina la kampuni hiyo baada ya kuwauliza wahusika.na kutoa wito kwa waandishi hao kuwasiliana na Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar.

Akielezea juu uokozi unavyoendelea amesema kuwa maiti tano zaidi zimepatikana hii leo na kufanya idadi ya waliofariki kuwa 197 na kazi ya uokoaji inaendelea.

Wakati huo huo Serikali ya Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa mchango wake wa maafa wa shilingi milioni mia tatu ambapo pia shilingi kumi na tatu milioni za msaada kama huo zimetolewa na Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa Tanzania (NSSF) na shilingi milioni kumi zimetolewa na Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF) pia kampuni ya simu ya Tigo imetoa chakula cha msaada chenye thamani ya shilingi milioni tano.

Aidha shilingi laki tano zimetolewa na mwananchi ambae jina lake hakutaka litajwe kwa ajili ya kusaidia maafa hayo.ambapo pia kesho jioni kutakuwapo na kisomo maalum kilichotayarishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar cha kuwaombea dua waliofariki pamoja na waliofikwa na maafa hayo hapo katika kiwanja cha Maisara Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad