Rais
Jakaya Kikwete, akiwa ameongozana na Mama Salma Kikwete, akitoa pole
kwa ndugu, jamaa na marafiki alipowasili uwanja wa Maisara Zanzibar jana
jioni kujiunga na Watanzania katika kuomboleza msiba huu mzito kwa
Taifa la Tanzania
Na Mwandishi Maalumu
KUFUATIA
msiba mkubwa uliotokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander
katika bahari ya Hindi usiku wa kuamkia Jumamosi, Septemba 10, 2011,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete, ameamuru maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu kuanzia
leo tarehe 11 Septemba, 2011 ambapo bendera nchini zitapepea nusu
mlingoti.
Aidha,
kufuatia msiba huo, Mheshimiwa Rais, ameahirisha ziara rasmi ya
kiserikali ya siku tatu nchini Canada ambako alikuwa amealikwa na Gavana
Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.
Katika
ziara hiyo iliyokuwa ifanyike kuanzia tarehe 14 – 16 Septemba, 2011,
Mheshimiwa Rais angekutana pia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa
Stephen Harper. Mheshimiwa Rais ameiomba Serikali ya Canada kupanga
ziara hiyo kwa tarehe za baadaye.
Rais
alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar,
kuwajulia hali, baada ya ajali hiyo. Akiwa katika ziara hiyo ya majonzi
aliarifiwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa imechukua
maamuzi kadhaa kukabiliana na hali ya ukoaji wa watu katika ajali hiyo.
Miongoni
mwa hatua hizo ni pamoja na kuchangia kiasi cha sh. milioni 300 ili
kusaidia zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kusaidia kusafirisha na kuzika
miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo. SMZ imetoa sh
milioni 100 kwa shughuli hiyo.
Serikali
ya Muungano pia imeamua kukubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika
Kusini kwa ajili ya kusaidia kufanya tathmini ya jinsi meli ilivyozama
na kuokoa maisha ya watu ambao watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Aidha
leo, Septemba 11, 2011, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama itafanya
kikao chake mjini Zanzibar kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya
kupata maelezo kamili kuhusu ajali hiyo, kupokea ripoti ya ajali,
kufanya tathmini ya ripoti hiyo na kutoa maelekezo ya jinsi ya
kukabiliana na hali ya sasa na hali ya baadaye ya usafiri wa maji
nchini.
Hata hivyo kabla ya kikao hicho, tayari Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajili hiyo.
No comments:
Post a Comment