Meneja wa Benki ya Exim Tanzania Tawi la Temeke James Nzalalila (kulia) akikabidhi sehemu ya vifaa vya usafi kwa Ofisa Afya wa Soko la Stereo Leonard Chigalula baada ya wafanykazi wa benki hiyo kushiriki kusafisha soko la Stereo lililopo Temeke Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kama sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo katika shughuli za kijamii nchini.
Wafanyakazi wa Benki ya Exim Tanzania kutoka matawi mbalimbali ya Dar es Salaam wakishiriki kusafisha soko la Stereo lililopo Temeke Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kama sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo katika shughuli za kijamii nchini.
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim Tanzania imeunga mkono mkakati wa usafi wa mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa kushiriki kusafisha Soko la Stereo lililopo Temeke Dar es Salaam.
Wafanykazi wa matawi mbalimbali ya benki hiyo yaliyopo Dar es Salaam waliunganisha nguvu na kushiriki katika usafi wa jumla wa soko hilo ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wao kama benki kwa jamii.
Akizungumza wakati wa usafi huo, Meneja Mkuu wa benki hiyo Dinesh Arora alisema pamoja na usafi benki hiyo imepata nafasi ya kujionea mazingira halisi ya soko hilo na kwamba wataangalia uwezekano wa kuyaboresha.
Alisema pamoja na maeneo mengine,sehemu ambayo imewagusa na kuona haja ya kuifanyia kazi ya haraka kama benki ni jinsi ya kuwafikia wafanyabiashara husika na kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kunufaika na mikopo ya benki hiyo.
Alisema biashara nyingi zinazoendeshwa katika masoko zimekuwa katika mazingira magumu ya kuwakomboa wahusika hivyo ipo haja kwa taasisi za kibenki kuliangalia hilo katika kuwawezesha kimtaji na Exim wapo tayari kufanya hivyo.
"Tumekuja kuangalia mazingira halisi ya soko pamoja na kupata picha ya biashara zinazoendeshwa ndani ya soko hili ili kama benki tuone jinsi tunavyoweza kushiriki kuwakomboa wahusika",
"Lakini pamoja na hilo tuliona haitakuwa busara kwetu kuja na kuondoka bila kuonyesha uwajibika kwa jamii hii, hivyo tumeshiriki kusafisha maeneo mbalimbali ya soko na tunaahidi kufanya hivi kila mara tutakapokuwa tunapata wasaa wa kufanya hivyo", alisema Arora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo Rajabu Kingalu aliishukuru benki hiyo kufanya ziara katika soko hilo na kufungua milango ya ushirikiano kati yao na benki.
Alisema pamoja na mambo mengine wamekuwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha soko hilo linakuwa katika mazingira ya usafi na kwamba kutembelewa na wadau kama taasisi za kifedha ni ishara ya nyota njema kwao katika usafi.
Kwa upande wa uwezeshwaji katika mitaji kupitia mikopo alisema taratibu ngumu za urejeshaji mikopo husika zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara hususani wa masokoni kwani biashara zao sio za mitaji mikubwa.
"Tumefarijika kuona taasisi ya kifedha kama benki imekumbuka na kuja kushiriki nasi katika usafi, tunaamini ujio wenu unaweza kutupa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto tunazozipata katika suala la usafi hapa sokoni",
"Pamoja na hili lazima tuchukue nafasi hii kuomba ushirikiano na benki yenu katika kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili biashara zetu ziweze kuinuka,milango ipo wazi karibuni", alisema Kingalu.
No comments:
Post a Comment