HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 7, 2011

MHE. WILLIAM LUKUVI AZUNGUMZIA KUHUSU TAARIFA YA HALI YA DAWA ZA KULEVYA YA MWAKA 2009

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE) MHE. WILLIAM V. LUKUVI

Tarehe 17/02/2011 niliwasilisha Bungeni, Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini ya mwaka 2009. Taarifa kama hii huwasilishwa bungeni kila mwaka na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa mujibu wa kifungu namba sita (6) cha Sheria namba tisa (9) ya mwaka 1995 ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.

Taarifa hii pamoja na mambo mengine inaelezea mwelekeo wa tatizo la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Pia, inatoa mapendekezo kwa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Taarifa hii inaainisha na kufafanua aina mbalimbali za dawa za kulevya, pamoja na madhara yatokanayo na matumizi yake. Pia, matatizo, changamoto na mikakati ya baadae ya kudhibiti dawa za kulevya imeainishwa. Vilevile, inaelezea juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali katika kupambana na tatizo hilo. Aidha, inaonyesha takwimu za ukamataji, kilimo na uteketezaji wa mashamba ya bangi.

Pia, taarifa inabainisha kwamba tatizo hili linaongezeka kwa kiwango kikubwa hapa nchini. Kwa mfano, mwaka 2009 kiasi kipatacho kilo 8.9 za heroin na kilo 4.4 za cocaine zilikamatwa ukilinganisha na kilo 3.7 za heroin na kilo 3.5 za cocaine zilizokamatwa mwaka 2008.

Halikadhalika, kiasi cha ekari 79 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika maeneo mbalimbali nchini mwaka 2009, ikilinganishwa na ekari 72 zilizoteketezwa mwaka 2008. Pamoja na hayo watuhumiwa wa dawa za kulevya kwa mwaka 2009 walikuwa 4,004 kati yao 263 walikuwa wanawake, wakati mwaka 2008 watuhumiwa walikuwa 6,606 kati yao 380 walikuwa wanawake.

Hali hii inaashiria kwamba watuhumiwa walikuwa wanakamatwa na kiasi kikubwa zaidi cha dawa za kulevya, na kwa upande mwingine inaonyesha kuwa wanawake pia wanajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Napenda kuwakumbusha wananchi kuwa matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa Taifa, kiuchumi, kiafya na kijamii. Vilevile, nachukua nafasi hii kuwapongeza watendaji wetu wa vyombo vya udhibiti na mashirika yote ya ndani na nje yanayoshiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Utendaji wao umefanikisha kujenga na kulinda heshima ya Tanzania kama nchi isiyovumilia siyo tu biashara bali pia matumizi haramu ya dawa za kulevya. Naviagiza vyombo vya dola viongeze jitihada za udhibiti. Nanyi waandishi wa habari nawaomba muendelee kuhabarisha umma kuhusu masuala ya dawa za kulevya.

Vilevile, nawasihi wananchi mtoe ushirikiano kwa vyombo vya dola pindi mnapopata taarifa za uzalishaji na biashara ya dawa za kulevya. Na mwisho nawasihi wadau wote kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi ili kuzuia Taifa letu lisitumbukie zaidi katika janga hili la dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad