***************************************************
Waandishi Wetu.
MWANANCHI
KUNUNUA HISA ZA RITES, KUITAFUTIA MBIA MWINGINE
SERIKALI itachukua hisa zake kutoka kwa mbia wake kwenye kampuni ya TRL, kwa lengo la kuzinunua hisa 51 za RITES katika kampuni hiyo ili kuinusuru kampuni hiyo iliyogubikwa na migogoro mingi.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Baraza la mawaziri ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la mawaziri, serikali imeamua kuzichukua hisa hizo ili kuiokoa kampuni hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
"Baraza la Mawaziri leo, (jana), katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, limejadili hali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kufanya maamuzi ya msingi kwa kukubaliana kama ifuatavyo maamuzi makuu mawili ya msingi,"alieleza Luhanjo.
Taarifa hiyo ya serikali imesema uamuzi wa kwanza wa msingi ni kwamba serikali ianze mara moja kujadiliana na RITES, mbia wa Serikali katika kampuni ya TRL, kwa lengo la Serikali kununua hisa 51 za RITES katika kampuni hiyo.
Uamuzi mwingine ni kwamba baada ya hapo, serikali ifanye matayarisho ya msingi ikiwa ni pamoja na kurekebisha kasoro na kuangalia mustakabali wa TRL, na kuiandaa kampuni hiyo kwa ajili ya kutafutiwa mbia mwingine wa kushirikiana na serikali katika kuendesha TRL.
Maamuzi hayo yanachukuliwa takribani siku tano baada ya Rais Kikwete kusema hatma ya shirika hilo kongwe ingejulikana juzi.
Kikwete alisema hayo mkoani Tabora alipokuwa akihutubia mamia ya watu wa kada tofauti kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi katika kilele cha maadhimisho ya Siku Wanawake Duniani.
Shirika hilo limekumbwa na matatizo makubwa ya kiundeshaji tangu serikali iingie ubia na kampuni ya Rites ya India na wafanyakazi wameonekana kutoikubali menejimenti mpya ambayo imekuwa ikishindwa kulipa mishahara kwa wakati, hali ambayo imekuza migogoro kutokana na kuwepo kwa migomo ya mara kwa mara.
Mbali na matatizo hayo ya kiundeshaji, shirika hilo lilikumbwa na matatizo zaidi baada ya kulazimika kusimamisha safari zake kutokana na mafuriko yaliyotokea katika mikoa ya Morogoro na Dodoma kuharibu miundombinu ya reli.
Hali ya shirika hilo limekuwa mjadala wa wadau mbalimbali lakini halikuweza kujadiliwa kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutokana na kile kilichoelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa taarifa zake zilikuwa hazijaiva na sasa litawasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge uliopangwa kufanyika Aprili.
Serikali ilisaini mkataba wa miaka 25 na Rites Oktoba 2007 ikiwa na matumaini mengi ya kuboresha huduma za usafiri wa reli ambao umekuwa muhimu kwa maisha ya wananchi waishio mikoa ya kati na Kanda ya Ziwa pamoja na uchumi wa taifa.
Kuzorota kwa shirika hilo kumeongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa maeneo hayo kutokana na bidhaa mbalimbali, yakiwemo mafuta kupanda bei huku taifa likipoteza mabilioni ya fedha yatokanayo na usafirishaji wa mizigo kwenda mikoa hiyo na nchi jirani.
TRL ni shirika linaloendeshwa kwa ubia baina ya serikali, inayomiliki asilimia 49 ya hisa, na kampuni ya Rites ya India inayomiliki asilimia 51.
Tatizo viongozi wetu wabishi kama KIMBA, Tulishawaeleza ao si wawekezaji lakini ndio mambo yetu ya mshiko mbele, atakama ujui ulifanyaro ukishatoa pesa basi wewe utashinda
ReplyDelete