*Asisitiza mifumo iliyozinduliwa ifanye kazi kwa ufanisi na kuendana na mahitaji ya wateja
*Aipongeza TANESCO kwa ubunifu na kuimarisha huduma kwa wateja wakubwa
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Oktoba 6, 2026 amezindua Mkataba wa Huduma kwa Wateja uliohuishwa pamoja na huduma mbalimbali za TANESCO zinazolenga kuboresha zaidi namna ya utoaji wa huduma kwa wateja kwa ufanisi na kwa wakati, uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Homera amesema matumizi ya mifumo ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma kwa wateja yanazidi kuiwezesha TANESCO kupiga hatua kubwa katika kuboresha huduma zake kwa kuzingatia uwajibikaji, uwazi na weledi unaolenga kuleta matokeo chanya kiutendaji.
Ametoa rai kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi katika matumizi ya umeme zinashughulikiwa kwa haraka kwa kuwa changamoto katika huduma ya umeme zinaweza kuathiri moja kwa moja uzalishaji na shughuli za kiuchumi.
“Mwelekeo wa Serikali ni kujenga sekta ya nishati inayoweza kuunga mkono kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Tunataka kuona shughuli za uzalishaji zinaendelea bila vikwazo visivyo vya lazima na tunataka wananchi wapate huduma kwa urahisi zaidi,” ameeleza Waziri Homera.
Amesema Tanzania hivi sasa ina umeme wa kutosha, ambapo uwezo wa uzalishaji umefikia jumla ya Megawati 4,606 dhidi ya mahitaji ya juu ya Megawati 2,316, hatua inayotoa fursa zaidi za kukuza shughuli za kiuchumi kupitia uwekezaji katika viwanda, biashara na shughuli za kijamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kuja na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika nyanja mbalimbali.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema Bodi itaendelea kuisimamia TANESCO katika kuhakikisha utoaji wa huduma unaenda sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa, ili huduma zimfikie mteja moja kwa moja bila vikwazo.
“Bodi itaendelea kuishauri TANESCO katika utoaji wa huduma kwa ufanisi. Kwetu sisi, mteja ni mfalme, na huduma inayotolewa na Shirika inamgusa mwananchi moja kwa moja. Tumejipanga kuhakikisha jitihada hizi zinaendelea kupiga hatua,” amesisitiza Balozi Bundala
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, ametoa ufafanuzi kuhusu uzinduzi wa Twiga Assistant, mfumo unaolenga kuachana na utoaji wa huduma kwa njia za makaratasi na kuingia katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki inayompunguzia mteja kutumia muda mrefu kusubiri huduma anayohitaji.
“TANESCO inafanya kazi kubwa kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi baada ya kukamilika kwa miradi mingi ya kimkakati, ukiwemo Mradi wa Chalinze–Dodoma. Hatua hii inatupa nguvu ya kuja na ubunifu wa kuona namna ya kumfikia mteja kwa haraka.
Ndiyo maana TANESCO imeamua kushuka chini na kusogeza huduma zake karibu na wananchi,” amefafanua Bw. Twange.
Hafla hiyo iliyobeba kaulimbiu ya “EXTRA MILE” imeenda sambamba na uzinduzi wa namba mpya ya 185 kwa ajili ya wateja wakubwa, Twiga AI Chatbot, mfumo saidizi wa kidijitali unaolenga kujibu maswali ya wateja, Kitengo cha watwja wakubwa kilichoboreshwa, pamoja na Premium Customer Portal, mfumo maalumu kwa ajili ya wateja wakubwa, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika shughuli za Shirika.
Uzinduzi huo umefanyika katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, ikiwa ni sehemu ya jitihada za TANESCO kuendelea kuboresha huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuhakikisha mteja anapata huduma kwa urahisi, haraka na kwa ufanisi.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment