
Na Karama Kenyunko Michuzi tv
KATIBU Mtendaji Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Katibu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (UNEP), Elizabeth Mrema, amesema taka za plastiki ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri afya ya bahari, akisisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutupa taka hizo baharini.
Mrema amesema hayo leo Oktoba 6, 2026 wakati wa Mkutano wa Waratibu wa Kitaifa na Washirika wa COP12, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Mrema amesema bahari ni muhimu kwa maisha ya binadamu kwa kuwa hutoa chakula na rasilimali nyingine muhimu, hivyo uchafu wa plastiki unapojazana baharini husababisha madhara kwa samaki na mimea ya baharini.
“Samaki wanameza, na ndio wanakufa,” amesema Mrema, akisisitiza umuhimu wa kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutupa chupa na taka nyingine za plastiki katika mazingira.
Amesema suala la usafi wa bahari si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi.
“Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa matendo yao ya leo yanaweza kuathiri maisha yao, watoto wao na vizazi vijavyo,” amesema.
Mrema pia amesema elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na makundi yote, wakiwemo wavuvi na watu wanaoishi katika maeneo ya mwambao, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira ya bahari.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Hamza Hassan Juma, amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua za vitendo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa bahari, upotevu wa bioanuwai na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za baharini.
Juma amesema mwaka huu unaadhimisha miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi, ikiwa ni miaka 40 ya ushirikiano, kujifunza na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuwa na Bahari ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi yenye afya na tija.
Amesema Tanzania inajivunia urithi wake wa maeneo ya pwani na visiwa, ikiwamo mwambao wa Dar es Salaam na visiwa vya kihistoria vya Zanzibar, ambavyo vina historia ya utunzaji wa bahari, biashara ya majini, utamaduni wa Kiswahili na uhusiano wa karibu kati ya watu na bahari.
“Urithi huu unatukumbusha kuwa bahari si rasilimali ya mazingira pekee, bali pia ni chanzo cha maisha, utamaduni, utambulisho na fursa za kiuchumi kwa watu wetu,” amesema.
Juma amesema pamoja na kusherehekea mafanikio yaliyopatikana katika miaka 40, nchi wanachama zinatambua changamoto zinazoukabili bahari, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa bahari, upotevu wa bioanuwai na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za baharini.
Amesema miaka 40 ijayo inapaswa kuwa ya kuimarisha ushirikiano, kuchukua hatua za vitendo na kupata matokeo yatakayogusa maisha ya watu na kuonekana katika bahari.
Mkataba wa Nairobi ulipitishwa Juni 21, 1985 na kuanza kutumika Mei 30, 1996. Tanzania iliuridhia Machi 1, 1996 na baadaye kuridhia Mkataba uliorekebishwa Septemba 4, 2017.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 wanachama wa Mkataba huo, pamoja na Comoro, Ufaransa, Kenya, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Somalia na Afrika Kusini.
Katika kipindi cha miaka 40, Mkataba huo umewezesha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi wa bahari, ikiwamo maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa, mipango ya kikanda ya kukabiliana na uchafuzi, ulinzi wa bioanuwai na kuimarisha uwezo wa kisayansi.
Tanzania imekuwa sehemu ya safari hiyo kupitia Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, kilichoanzishwa mwaka 1996, ambacho kilisimamia kutangazwa kwa Hifadhi ya Bahari ya Mnazi Bay–Ruvuma Estuary mwaka 2000 na Hifadhi ya Bahari ya Tanga Coelacanth mwaka 2009.
Juma pia amewakaribisha wajumbe wa COP12 kutembelea Zanzibar, akisema kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar ni dakika 20 kwa ndege au dakika 90 kwa kivuko cha mwendokasi.
Amesema ziara hiyo itawapa fursa ya kufurahia utamaduni na vivutio vya utalii vya Zanzibar wakati watakapokuwa nchini.



.jpeg)
No comments:
Post a Comment