HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 19, 2026

Uwekezaji Bandari ya Mtwara Wafungua Fursa za Kiuchumi



Mwandishi Wetu
WAKATI shehena ya mizigo mbalimbali ikiendelea kuongezeka katika Bandari ya Mtwara, wadau wa usafirishaji na wananchi wamesema hali hiyo imefungua fursa mbalimbali za kiuchumi.

Fursa hizo zinatokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikiwamo upanuzi wa gati uliowezesha meli kubwa kutia nanga kupakia na kushusha mizigo mbalimbali.

Mizigo hiyo ni pamoja na magari makubwa, vifaa vya ujenzi wa miradi ya kimkakati, saruji na mazao kama korosho, huku hali hiyo ikielezwa kupunguza gharama za usafirishaji kwenda nchi jirani ikiwamo Malawi, Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Msumbiji.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Hekima Ngezi, alisema bandari hiyo iliyoanzishwa mwaka 1950 imeboreshwa kwa kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena kubwa.

Ngezi alisema awali bandari hiyo ilikuwa ya msimu, ikitegemea zaidi karanga na baadaye korosho, lakini Serikali iliona umuhimu wa kuiongezea uwezo ili ifanye kazi mwaka mzima.

Alisema gati zimeongezwa kutoka tatu hadi nne, huku gati moja likiwa na urefu wa mita 300 na kina cha maji cha mita 13, hali inayowezesha meli kubwa kutia nanga na kupakia au kushusha shehena nyingi zaidi.

“Mpaka sasa, Bandari ya Mtwara inahudumia shehena ya mafuta, korosho, makaa ya mawe, mbaazi na saruji na tunahudumia magari makubwa. Kuanzia Februari mwaka huu hadi sasa, tumehudumia meli 23 na magari 6,390,” alisema.

Ngezi alisema Serikali inaendelea kujenga gati jipya katika eneo la Kisiwa Mpangawe/Kisiwa Mgao, lenye urefu wa mita 300 na kina cha maji mita 15, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 44 na linatarajiwa kukamilika mwakani.

Alisema gati hilo litatumika kuhudumia mizigo yenye asili ya vumbi, ikiwamo saruji na makaa ya mawe, na litaongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena nyingi zaidi.

Ngezi alisema Bandari ya Mtwara ipo katika Ushoroba wa Kusini unaounganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma, hivyo ina nafasi muhimu katika kukuza biashara ya ndani na kuvuka mipaka.

Kwa upande wa wananchi, mama lishe Rehema Mputa alisema maboresho ya bandari yameongeza biashara na kipato chake, akieleza kuwa ameweza kumsomesha mtoto wake hadi kidato cha nne kupitia biashara hiyo.

“Yaani mimi kipindi hicho biashara ilikuwa ngumu sana hapa, lakini mpaka leo nimemsomesha mtoto wangu amemaliza kidato cha nne kwa fedha hizi hizi za mama lishe,” alisema.

Naye dereva wa bodaboda, Issa Mchika, alisema shughuli za bandari zimeongeza abiria na kipato kwa madereva kutokana na ongezeko la magari ya mizigo, mafuta na wageni wanaofika Mtwara.

Kwa upande wake, Wakala wa Baruti International Limited, Abdulrahman Upete, alisema maboresho ya bandari yameongeza ufanisi na kuifanya Mtwara kuwa kiungo kwa nchi zinazozunguka Tanzania.

Upete alitaka Serikali iendelee kuwekeza katika mitambo na miundombinu, huku akiwataka wananchi kuchangamkia fursa za udereva na huduma zinazohusiana na usafirishaji.

Wakala wa Meli wa Joyous Shipping Service Ltd, Esthersia Mallya, alisema mazingira ya Bandari ya Mtwara yamebadilika, huku idadi ya meli ikiongezeka na huduma kutolewa kwa wakati.

“Uboreshaji ambao umefanyika pamoja na mifumo ya namna ya kuhifadhi mizigo inavutia kuitumia, kiasi kwamba mzigo wako utakavyoingia ndivyo utakavyoupata,” alisema.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad