Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amepongeza ubunifu ulioonyeshwa na wanafunzi wa Chuo cha St Joseph jijini Dar es Salaam, akisema ukiendelezwa unaweza kutatua changamoto nyingi zinazoikabili jamii.
Amesema Serikali itashirikiana na vyuo binafsi kuhakikisha masomo ya sayansi yanapewa kipaumbele ili kupatikane wahandisi wengi nchini na kuondoa utegemezi wa wataalamu wa kigeni. Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza kwenye Wiki ya Tafiti na Ubunifu ya Chuo cha St Joseph, ambapo wanafunzi walionyesha ubunifu wa teknolojia mbalimbali za uhandisi.
Profesa Mkumbo alisema chuo hicho kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kutoa wataalamu wa sayansi na kukitaka kuendelea kuchukua nafasi yake miongoni mwa vyuo vinavyotoa wataalamu wengi wa fani hiyo nchini. Alisema ametembelea maonesho ya kitaaluma ya wanafunzi na kubaini kuwa wamebuni vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa na manufaa kwa taifa.
“Nimejionea ubunifu mkubwa sana kwa wanafunzi wenu, lakini kinachosikitisha ni kuwa ubunifu huo unaishia kuwa wazo tu, haufikii mwisho. Nawapa changamoto mhakikishe ubunifu wa wanafunzi wenu unaunganishwa na viwanda na kuwa halisi,” alisema.
“Haitakuwa na maana kama mtakuwa mnabuni vitu lakini vinaishia kwenye vyuo vyenu. Lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha mnatumia bunifu hizo kuzalisha, wanafunzi wakimaliza hapa wanakwenda kujiajiri au kuajiriwa,” alisema.
Alisema wanafunzi wa vyuo vya sayansi wanapaswa kuendelea kubuni vitu nafuu vitakavyosaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii, akieleza kufurahishwa na ubunifu wa wanafunzi hao wa kutumia nishati safi ya kupikia majumbani wakati ambapo nishati hiyo imekuwa ajenda ya Serikali.
“Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanatumia nishati safi ya kupikia. Kwa hiyo nilipoona nanyi mmebuni matumizi ya nishati safi nilifurahi sana, nawapongeza sana,” alisema.
Aidha, alimpongeza Makamu Mkuu wa chuo hicho na menejimenti kwa kuanzisha vituo vitano vya uhamiri vinavyofundisha masuala ya sayansi katika maeneo mbalimbali nchini. “Mnapojikita kwenye matumizi ya roboti na akili mnemba mnakwenda sambamba na dunia inakoelekea kwa sasa. Serikali inakwenda kutekeleza Dira 2050 na moja ya mambo yanayozingatiwa ni matumizi ya teknolojia,” alisema.
Alimpongeza mwanzilishi wa chuo hicho kwa uamuzi wa kuanzisha chuo nchini wakati sekta binafsi haikuwa imekubalika kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa. Alisema St Joseph ni miongoni mwa vyuo vinavyoongoza katika kufundisha masomo ya sayansi na kuwataka viongozi wake kuhakikisha kinaendelea kuwa kinara katika eneo hilo.
“Kwenye vyuo vinavyofundisha masomo ya sayansi St Joseph mnaongoza, kwani ndio mlianza kufundisha masomo haya kabla ya wengine. Naomba mhakikishe mnabaki kwenye nafasi yenu ya kuwa kinara wa kufundisha masomo ya sayansi,” alisema.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment