HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 17, 2026

MAWAZO YA BUNIFU YA WANAFUNZI WA TIA YAWA CHANZO CHA VIJANA KUJIAJIRI

 


Na Mwandishi Wetu, Tanga
MAWAZO ya ubunifu na teknolojia yanayobuniwa na wanafunzi na wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yameelezwa kuwa ni fursa muhimu kwa vijana kujiajiri, huku yakitoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Miongoni mwa wabunifu hao ni Calven Mwakampya, mhitimu wa TIA ambaye amebuni kifaa cha teknolojia kinachoitwa Smart Glove, kinachowezesha mawasiliano kati ya mtu mwenye uziwi na asiye na uziwi.

Mwakampya amebuni mfumo unaotumia vitufe vya alama za mawasiliano, ambapo ujumbe unaowasilishwa na mtu mwenye uziwi unaweza kubadilishwa kuwa sauti na kusikika kwa mtu asiye na uziwi, hivyo kusaidia kuondoa changamoto ya mawasiliano kati ya makundi hayo.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Mwakampya alisema ubunifu huo wa kiteknolojia umemsaidia kutengeneza suluhisho la changamoto ya mawasiliano inayowakabili watu wenye uziwi.

Alisema amekuwa miongoni mwa wahitimu walionufaika na mpango wa TIA wa kukuza na kuendeleza vipaji na taaluma, jambo lililomsaidia kuboresha wazo lake na hatimaye kuanzisha kampuni.

"Nimekuwa miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika na mpango wa TIA wa kukuza na kuendeleza vipaji na taaluma, jambo linalonisaidia kuendeleza wazo ambalo sasa tumeanzisha kampuni," alisema Mwakampya.

Alisema TIA imekuwa ikimpa mwongozo na usimamizi katika kuboresha ubunifu huo, ambao umeanza kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili watu wenye uziwi katika mawasiliano.

Kwa mujibu wa Mwakampya, mfumo huo utamwezesha mtu mwenye uziwi kuwasiliana na mtu asiye na uziwi kwa urahisi, huku ujumbe wa alama ukibadilishwa kuwa sauti ili kumwezesha mtu asiye na uziwi kuelewa mahitaji ya anayewasiliana naye.

Alisema mfumo huo pia utasaidia kuongeza ufanisi wa mawasiliano kati ya jamii ya watu wenye uziwi na wasio na uziwi katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.

Mwakampya alisema matumizi ya teknolojia katika sekta ya mawasiliano ni muhimu katika kuhakikisha watu wenye uziwi wanapata na kutoa huduma kwa ufanisi kama ilivyo kwa watu wasio na uziwi.

Aidha, alisema mpango wa TIA wa kuendeleza mawazo na ubunifu wa wanafunzi una nafasi kubwa katika kuongeza fursa za ajira, hususani kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali.

"Ubunifu unaotokana na wanafunzi unaweza kuwa chanzo cha kujiajiri na pia kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa," alisema.

Alitoa wito kwa vijana kutumia maarifa wanayopata vyuoni kubuni teknolojia na bidhaa zitakazokuwa na manufaa kwa jamii, badala ya kutegemea ajira baada ya kumaliza masomo.

"Ninatoa wito kwa vijana kutumia maarifa wanayopata vyuoni kubuni teknolojia zitakazokuwa na manufaa kwa jamii," alisema Mwakampya.

Alisema miongoni mwa wadau wanaoweza kunufaika na teknolojia hiyo ni TIA kwa ajili ya kusaidia katika ufundishaji wa watu wenye uziwi, Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), hospitali na maeneo mengine ya kutolea huduma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad