HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 17, 2026

TEA: MKONDO WA AMALI WAZIDI KUPATA MWITIKIO KWA WANAFUNZI

 



Na Mwandishi Wetu, Tanga
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imesema mkondo wa Amali katika shule za sekondari umeendelea kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa wanafunzi kutokana na upatikanaji wa vifaa vinavyowawezesha kujifunza kwa vitendo.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Afisa Miradi wa TEA, Kabula Julu, alisema shule zilizofadhiliwa vifaa kwa ajili ya mkondo wa Amali zimeanza kushuhudia ongezeko la hamasa miongoni mwa wanafunzi.

Alisema miongoni mwa shule zilizonufaika na ufadhili huo ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, ambayo imepatiwa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 400 kwa ajili ya kufundishia fani tano.

Alizitaja fani hizo kuwa ni Upishi, Kilimo cha Mboga na Matunda, Ushonaji, Kilimo cha Mazao ya Chakula pamoja na Afya ya Wanyama.

Julu alisema shule nyingine zilizonufaika na ufadhili wa TEA ni pamoja na Uwemba, Iringa, Kigoma, Dar es Salaam, Arusha, Chief Salwart ,Morongo pamoja na Korogwe.

Alisema miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na TEA ni kufadhili shule zenye mkondo wa Amali, ambao umekuwa ukipata mwitikio mkubwa kutokana na kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi badala ya kutegemea nadharia pekee.

"Tumefadhili shule zenye mkondo wa Amali na mwitikio umekuwa mkubwa, kwa sababu wanafunzi wana uhitaji wa kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia," alisema Julu.

Aliongeza kuwa ushiriki wa TEA katika maonesho hayo unatoa fursa kwa wananchi kufahamu namna Mamlaka hiyo inavyoshiriki kuboresha mazingira ya elimu na kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia katika maisha na kujiajiri.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Catherine Machugu, alisema ufadhili wa TEA umeongeza chachu kwa wanafunzi kupenda na kusoma mkondo wa Amali.

Alisema kabla ya shule hiyo kupata vifaa, wanafunzi walikuwa wakijifunza zaidi kwa nadharia, lakini baada ya kupata vifaa wameanza kujifunza kwa vitendo na matokeo yameanza kuonekana.

"Wakati tulipokuwa hatuna vifaa, wanafunzi walijifunza zaidi kwa nadharia, lakini kwa sasa wanajifunza kwa vitendo na matokeo yanaonekana," alisema Machugu.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad