.jpeg)
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MIXX imewakutanisha wajasiriamali 18 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kupanua masoko.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kanda ya Kusini ya Dar es Salaam wa MIXX by YAS, Robert Kasulwa, alisema wajasiriamali hao ni wanufaika wa awamu ya pili ya mradi wa Anzia Ulipo, unaolenga kuwawezesha Watanzania kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali.
Kasulwa alisema katika awamu hiyo, jumla ya wajasiriamali 48 wamenufaika na mafunzo pamoja na uwezeshaji wa biashara, huku 18 kati yao wakipata nafasi ya kushiriki maonesho ya Sabasaba ili kutangaza bidhaa zao na kukutana na wateja pamoja na wadau mbalimbali wa biashara.
Alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwainua kiuchumi kwa kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara endelevu katika maeneo mbalimbali nchini.
"MIXX by YAS inaendelea kushirikiana na wajasiriamali kwa kuwapa fursa za kujifunza, kuonyesha bidhaa zao na kupanua mtandao wa biashara. Tunaamini uwezeshaji huu utachochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," alisema Kasulwa.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji wa wananchi kwa lengo la kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi na kutumia huduma za kifedha za kidijitali kukuza biashara zao.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment