KAMPUNI ya Ulinzi ya SGA Security imetajwa tena kuwa miongoni mwa watoa huduma za usalama wanaoaminika zaidi barani Afrika, baada ya kushinda Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji kwa mwaka 2025 (Consumer Choice Awards Africa 2025).
Tuzo hiyo ilitangazwa kwenye tamasha la mwaka la utoaji wa tuzo hizo lililofanyika katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na makampuni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Dkt. Eric Sambu, alisema ushindi huo unaonesha namna watumiaji wa huduma za ulinzi wanavyoendelea kuiamini kampuni hiyo, ambayo imekuwepo kwa muda mrefu katika bara la Afrika.
Hii ni miongoni mwa tuzo kadhaa ambazo kampuni hiyo imepata, ikiwamo ile ya Kampuni Bora ya Ulinzi ya Mwaka Afrika katika kundi la huduma za ulinzi.
Dkt. Sambu alibainisha kuwa kampuni imekuwa ikiboresha huduma zake ili kuhakikisha wateja wanapata thamani ya fedha na kuboresha mahusiano kati ya kampuni na wateja. Alisema tuzo hiyo pia inawakilisha kazi ya wafanyakazi zaidi ya 18,000 wa kampuni hiyo barani Afrika.
Alisema SGA ina vyeti vinne vya Shirika la Kimataifa la Kusanifisha (ISO), vinavyoonyesha uimara wa mifumo yake ya usimamizi katika kuhakikisha ubora wa huduma kwa wateja na umma.
Kwa mujibu wake, mafanikio ya kampuni hiyo yanatokana na uwekezaji katika mafunzo kwa wafanyakazi wake wa ngazi zote, hususan katika maeneo yanayohusu mwenendo, vitisho na mabadiliko katika sekta ya ulinzi.
Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji Afrika ni tukio la kila mwaka linalotoa heshima kwa makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali barani Afrika kupitia kura za mtandaoni zinazokusanywa kupitia tovuti iliyoanzishwa mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment