Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 3,799.22 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 18 za mashamba ya bangi na kutaifisha mali za wahalifu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.304. Aidha, jumla ya watuhumiwa 84 walikamatwa katika operesheni hizo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas James Lyimo amesema Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa uamuzi wa kutaifisha mali za watuhumiwa Saleh Khamis Basternan na Gaspar Beschi Faki baada ya kubainika kuwa walizipata kupitia biashara ya dawa za kulevya.
Mali zilizotaifishwa zinajumuisha nyumba, viwanja na magari mbalimbali.
DCEA imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazao ya Uhalifu (Sura ya 255), Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa (Sura ya 200) na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015.
Utaifishaji huo unalenga kuondoa mazalia ya uhalifu na kutoa funzo kwa jamii kuwa uhalifu hauna tija.
MALI ZILIZOTAIFISHWA
Mali zilizotaifishwa zinajumuisha:
Apartment QA2 Sea Breeze Residential Complex, Jangwani Beach
Apartment 6B, Kariakoo
Nyumba mbili Mbezi, Kinondoni
Viwanja mbalimbali vya Mbweni, Kigogo (Kisarawell), Shungubweni, Boza na Bagamoyo,magomeni
Apartment PA1 Sea Breeze Residential Complex
Magari 11 yakiwemo Nissan Civilian, Subaru Impreza, Toyota Spacio na Volkswagen.
Katika operesheni iliyofanyika Sinza D, watuhumiwa Cuthbert Kalokola (34) na Murath Abdallah (19) walikamatwa na vidonge 738 vya dawa aina ya MDMA (uzito gramu 177.78) na vidonge 24 vya dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol (gramu 10.03).
Eneo la Mbezi Maramba Mawili, watuhumiwa saba walinaswa wakisafirisha kilogramu 80 za dawa za kulevya aina ya skanka zilizokuwa zimefichwa ndani ya matanki ya solar panel kwenye basi la kampuni ya Falcon aina ya Scania, lenye namba T 372 DFK lililokuwa likitoka Malawi.
KUKAMATWA KWA KILO 244.5 RUKWA
Katika mpaka wa Kasesya, Rukwa, mtuhumiwa Godwin Andrew (26) mkazi wa Mbalizi – Mbeya alikamatwa na kilo 244.5 za skanka zilizokuwa zimefichwa ndani ya spika, CPU, mashine za kukatia majani na mashine za kupooza hewa. Mizigo hiyo ilisafirishwa kwa gari aina ya Iveco Van lenye namba za Afrika Kusini DN 65 FN GP mali ya Makamua Logistics Limited.
OPERESHENI MIKOANI
Katika mikoa mbalimbali, DCEA ilikamata kilo 2,041.45 za bangi, kilo 1,423.28 za mirungi na kuteketeza ekari 18 za mashamba ya bangi. Pia magari manne na pikipiki 12 zilinaswa katika operesheni hizo.












No comments:
Post a Comment