Mnufaika wa ufadhili wa Masomo ya Programu ya Shahada ya Uzamili ya Lugha ya Kiswahili katika Chuo Cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) Frank Kaswahili akipokea hundi ya Tsh 3,900,000 kutoka Kwa Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi (wa pili kulia. Wengine kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TATAKI Dr. Rhoda Kidami, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Prof. Baraka Maiseli na Meneja Rasilimali watu wa ALAF Limited, Jumbe Onjero. Hafla hiyo ilifanyika chuoni hapo leo Desemba 17,2025
WANAFUNZI watatu wa Shahada ya Uzamili ya lugha ya kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) wamepata ufadhili wa masomo kutoka Kampuni ya ALAF Limited.
Ufadhili huo umetangazwa leo Desemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa wanufaika hao watatu, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF LTD, Hawa Bayumi alisema hatua hiyo ni muendelezo wa juhudi za kampuni hiyo kukuza Kiswahili katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kote.
"Kiswahili ni moja ya tunu kubwa tuliyorithi kutoka kwa Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni lugha ambayo inazidi kuenea na kupata umaarufu duniani na hatimaye kutambulika kuwa ndiyo lugha itakayoleta mshikamano wa bara la Afrika, hivyo tumeona hatuna budi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuikuza lugha hii adhimu”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na jukumu kubwa na muhimu katika kuandaa na kutekeleza Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika, ambazo Kampuni ya ALAF LTD inadhamini pamoja na makampuni yake dada yaliyoko nchini Kenya na Uganda na ambayo inawaunganisha waandishi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
"Sisi kama moja wapo ya makampuni yaliyopata mafanikio makubwa na kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kama zana muhimu ya maendeleo ya kitamaduni, kijamii na kiuchumi, tumeona umuhimu wa kukuza fasihi ya Kiswahili na ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuikuza lugha hii”, alisema.
Aliwataja wanufaika wa ufadhili huo kuwa ni Frank John Kaswahili, Yasenta Emanuel Dagati, na Veromina Boazi Kerato ambapo jumla ya ufadhili huo ni Tsh 11,700,000.
Alitoa wito kwa wanufaika kutumia ufadhili walioupata vyema kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye masomo yao ili wawe na mchango mkubwa katika kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili kupitia elimu watakayoipata.
Kwa upande wake Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeishukuru kampuni ya ALAF kwa ufadhili huo ambao umesema kuwa ni sehemu ya maombi mengi yaliyofanywa na wanafunzi wengi.
"Kwa kawaida huwa kuna maombi mengi kutoka kwa wanafunzi kuhusiana na ufadhili huu lakini ni wanafunzi watatu pekee ndio wanaonufaika; kwa hili tunawashukuru sana ila tunaomba mfikirie jinsi ya kuongeza idadi ya wanufaika ili lugha ya Kiswahili iweze kukua zaidi", alisema Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Prof. Baraka Maiseli.

Mnufaika wa ufadhili wa Masomo ya Programu ya Shahada ya Uzamili ya Lugha ya Kiswahili katika Chuo Cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) Yasenta Dagati akipokea hundi ya Tsh 3,900,000 kutoka Kwa Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi (wa pili kulia. Wengine kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TATAKI Dr. Rhoda Kidami, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Prof. Baraka Maiseli na Meneja Rasilimali watu wa ALAF Limited, Jumbe Onjero. Hafla hiyo ilifanyika chuoni hapo leo Desemba 17,2025

Mnufaika wa ufadhili wa Masomo ya Programu ya Shahada ya Uzamili ya Lugha ya Kiswahili katika Chuo Cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) Veromina Kerato akipokea hundi ya Tsh 3,900,000 kutoka kwa Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi (wa pili kulia. Wengine kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TATAKI Dr. Rhoda Kidami, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Prof. Baraka Maiseli na Meneja Rasilimali watu wa ALAF Limited, Jumbe Onjero. Hafla hiyo ilifanyika chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment