
*Mkuu wa Gereza Apongeza Juhudi za Serikali.
* Asema Nguvu Kazi Sasa Inaelekezwa Kwenye Shughuli za Kiuchumi.
Tabora.
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imepanga kupeleka majiko matatu ya kisasa yanayotumia mkaa mbadala pamoja na sufuria zake katika Gereza la Kilimo Urambo, mkoani Tabora.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Bw. Nolasco Mlay, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Gereza la Kilimo Urambo ambapo alijionea utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mlay amesema Serikali kupitia REA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuziimarisha kwa miundombinu ya kisasa inayotumia teknolojia rafiki kwa mazingira kama majiko banifu na mifumo ya gesi.
Aidha, Bw. Mlay amesema Gereza la Mahabusu Urambo tayari limefungiwa mfumo mmoja wa gesi na kwa sasa linasubiri kupatiwa majiko manne ya gesi, Sambamba na hilo, gereza hilo pia litapatiwa majiko matatu yanayotumia mkaa mbadala ili kuendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika magereza nchini.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Gereza la Kilimo Urambo, Bw. Joseph Mzumara amepongeza juhudi za Serikali katika kuhakikisha taasisi na jamii kwa ujumla zinaachana na matumizi ya nishati zisizo salama kama kuni, ambazo zinaathiri afya na mazingira.
“Hapo awali tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa za kutafuta kuni maeneo ya mbali, lakini kwa sasa tunatumia mkaa mbadala. Hali hii imesaidia kupunguza muda unaotumika kutafuta nishati zisizo salama na badala yake nguvu kazi inaelekezwa kwenye shughuli nyingine za kiuchumi," amesema Mzumara
Aidha, ameishukuru Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia pia watumishi wa Jeshi la Magereza.
"Watumishi wote tumepatiwa majiko ya gesi yanayotuwezesha kupika kwa haraka na kutekeleza majukumu yetu mengine kwa ufanisi zaidi badala ya kutumia muda mwingi kutafuta nishati zisizo salama," amesema.
Ameongeza kuwa Gereza la Kilimo Urambo lina mifugo ya kutosha, na kwa siku zijazo linajipanga kuanza kuzalisha gesi vunde (biogas) ili kujiongezea vyanzo endelevu vya nishati safi ya kupikia.

No comments:
Post a Comment