SERIKALI imesema itaendelea kuboresha huduma za kijamii katika Mtaa wa Muungano, Kata ya Goba jijini Dar es Salaam, ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kikatiba wa robo mwaka Oktoba 19, 2025 Jijini Dar ves Salaam , Mwenyekiti wa Mtaa huo, Stanlaus Maduhu, amesema ujenzi wa Shule ya Sekondari Muungano umekamilika kwa zaidi ya asilimia kubwa na unatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2026.
Maduhu ameishukuru Serikali Kuu na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa kufanikisha ujenzi huo, huku akiwataka wananchi kuendeleza ushirikiano katika kuipa elimu kipaumbele, akitolea mfano mafanikio ya Shule ya Msingi Kurangwa.
Huduma za Maji
Meneja wa DAWASA, Victoria Masele, ameahidi kuhakikisha wakazi wote wa mtaa huo wanapata maji safi na salama, hususan maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Aidha, amesema watashughulikia bili zenye dosari na akawataka wananchi kulinda miundombinu ya maji.
Miundombinu ya Barabara
Kwa upande wa changamoto za barabara na vivuko, taarifa imeeleza kuwa TARURA inaendelea na utaratibu wa kuzitatua hatua kwa hatua kulingana na mpango wa utekelezaji wa miundombinu katika jiji hilo.
Ulinzi na Usalama
Kamanda wa Polisi Kata ya Goba, Christopher Mwalukuta, amesema uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia ushirikiano kati ya wananchi na jeshi la polisi, na akasisitiza kuendeleza amani na kutoa taarifa za wahalifu.
Hata hivyo, ameonya juu ya kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wenye umri wa miaka 5–7, akiwataka wazazi na walezi kuwa makini na ufuatiliaji wa watoto.
“Kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia katika kituo chetu cha kata. Ni wajibu wa jamii kulinda watoto,” amesema Kamanda Mwalukuta.






No comments:
Post a Comment