HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 3, 2025

Mantra Yaelekezwa Kuwashirikisha Watanzania Uchimbaji wa Urani

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janeth Lekashingo, ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania Limited, inayosimamia Mradi wa Uchimbaji wa Madini ya Urani katika Mto Mkuju, kuhakikisha kuwa Watanzania wanashirikishwa kikamilifu katika hatua zote za uchimbaji na uchakataji ili manufaa ya rasilimali hiyo muhimu ya taifa yawafikie wananchi wengi zaidi.

Akizungumza Oktoba 1, 2025, katika ziara yake wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, akiwa ameambatana na Kamati ya Kitaifa ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Lekashingo alisema dhamira ya Serikali ni kuona mnyororo mzima wa thamani wa urani unawanufaisha Watanzania kupitia ajira, mafunzo ya kitaalamu na fursa za kukuza ujuzi.

“Uchimbaji wa urani si mradi wa kampuni pekee, bali ni rasilimali ya taifa. Ni haki ya Watanzania kunufaika na madini haya adimu. Ni lazima kuhakikisha vizazi vya sasa na vijavyo vinapata matunda yake,” alisisitiza.

Aidha, aliitaka kampuni hiyo kuajiri Watanzania kwa wingi na kuwawezesha kupata mafunzo ya kitaalam ili waweze kuchukua nafasi ambazo mara nyingi huchukuliwa na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Pia aliwataka viongozi wa mradi kuwasilisha taarifa sahihi kuhusu maendeleo na changamoto zinazojitokeza, badala ya kuonesha picha isiyo halisi ya mafanikio.

Dkt. Lekashingo pia aliwakumbusha viongozi wa mradi kuhusu makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa Novemba 15, 2024, na kuwasilishwa kwa uongozi wa halmashauri, akisisitiza kuwa utekelezaji wake usicheleweshwe tena.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, aliitaka Mantra Tanzania Limited kuzingatia sheria na kanuni za ushirikishwaji, huku akiwasisitiza wanasheria wa kampuni hiyo kuwakumbusha wamiliki wa leseni za madini wajibu wao kwa taifa.

“Milango ya Serikali ipo wazi kwa wadau wa Sekta ya Madini. Waje kupata ushauri, mafunzo au kueleza changamoto zao. Lengo letu ni kuhakikisha sekta hii inaleta maendeleo ya kweli kwa taifa,” alisema Dkt. Numbi.

Viongozi wa Mantra Tanzania Limited waliishukuru Tume ya Madini pamoja na Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwa elimu na mwongozo walioupata, wakiahidi kufuata kikamilifu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kufanikisha maendeleo ya mradi na kuhakikisha manufaa yake yanawafikia Watanzania.









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad