Na Mwandishi Wetu.
Arusha, 1 Oktoba 2025: Tume ya Madini imeboresha mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini ili kurahisisha upatikanaji wa leseni na kupunguza urasimu kwa wachimbaji na wawekezaji, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na mapato ya serikali.
Akifungua mafunzo maalum kwa maafisa wa madini kutoka mikoa yote ya kimadini jijini Arusha, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume hiyo, Francis Kayichile, amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha leseni zinapatikana kwa muda mfupi endapo masharti yote yamezingatiwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini.
“Tumeona ni vyema kuwakutanisha maofisa leseni kutoka mikoa zaidi ya 30 ili tuweze kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya mfumo huu. Lengo ni kumrahisishia Mtanzania au mwekezaji kupata leseni bila kukumbana na urasimu,” alisema Kayichile.
Ameongeza kuwa maboresho hayo pia yanakusudia kudhibiti mianya ya upotoshaji na matumizi mabaya ya nafasi, ambapo mifumo ya TEHAMA inatarajiwa kuwa chachu ya uwazi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza baada ya kila maboresho na kuhakikisha huduma kwa wawekezaji zinaimarishwa.


“Kila maboresho huambatana na changamoto katika utekelezaji. Tuliona ni vyema kukutana na maafisa hawa ili kuyatolea ufumbuzi wa pamoja kwa lengo la kuboresha huduma,” alisema Mhandisi Swedi.
Amebainisha kuwa maboresho ya mfumo yamechangia kuongeza mapato ya serikali, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ya Madini ilikusanya zaidi ya Shilingi trilioni 1.07, ikivuka lengo la awali la kukusanya Shilingi bilioni 999.

Washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza maboresho ya mfumo, wakisema yameondoa changamoto nyingi zilizokuwepo awali. George Mchiwa, Mjiolojia kutoka mkoa wa Songwe, alisema mfumo mpya umeboresha upatikanaji wa leseni na kuongeza uwazi.
“Mafunzo haya yatasaidia kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunazingatia sheria na taratibu zilizopo,” alisema.
Aidha, maafisa leseni waliokuwepo walibainisha kuwa elimu kwa wachimbaji na wawekezaji kuhusu umuhimu wa leseni inaendelea kutolewa, hatua ambayo imesaidia kudhibiti uchimbaji holela na kuongeza pato la serikali.

No comments:
Post a Comment