Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kung’ara katika ukusanyaji mapato baada ya kufanikisha ukusanyaji wa Shilingi Trilioni 8.97 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai – Septemba 2025).
Kiasi hicho kimezidi lengo lililowekwa la Shilingi Trilioni 8.44 kwa ufanisi wa asilimia 106.3 na kuashiria ongezeko la ukuaji wa mapato kwa asilimia 15.1 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 7.79 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 2, 2025 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda imesema mafanikio haya yamekuwa matokeo ya maboresho ya kimfumo, ushirikiano wa karibu na walipakodi, na sera nzuri za kiuchumi zinazowekwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika robo hii ya kwanza, makusanyo ya mwezi Julai yalifikia Sh. Trilioni 2.68 sawa na ufanisi wa asilimia 104.1, Agosti Sh. Trilioni 2.82 kwa ufanisi wa asilimia 110, na Septemba ikawa kilele kwa TRA baada ya kufanikisha makusanyo ya Sh. Trilioni 3.47 — kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa kwa mwezi mmoja katika historia ya mamlaka hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa makusanyo ya sasa yanaashiria ongezeko kubwa tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani mwaka 2021.
"Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21, TRA ilikusanya Sh. Trilioni 4.40 pekee katika robo ya kwanza, huku wastani wa makusanyo kwa mwezi ukiwa Sh. Trilioni 1.47. Hali ilivyo sasa, wastani wa makusanyo kwa mwezi umeongezeka mara mbili hadi Sh. Trilioni 2.99." Imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo imetaja mambo kadhaa yaliyosababisha mafanikio hayo, ikiwemo kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari bila uonevu, kuimarisha huduma kwa walipakodi kupitia "Dawati la Uwezeshaji Biashara", na kuanzisha programu ya "Mabalozi wa Kodi" ambayo imeimarisha mahusiano kati ya TRA na walipakodi.
Vilevile, muitikio wa wafanyabiashara wa mtandaoni, hususan wanaotoa huduma za malazi, umechangia kuongeza mapato kutokana na kampeni maalum za usajili na ulipaji kodi.
Aidha, matumizi ya mifumo ya kidigitali kama TANCIS na mashine za kielektroniki za EFD yameboresha uwazi na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwaTRA sasa imeweka mikakati ya kutoa huduma bora zaidi, ikiwemo kuwahudumia walipakodi hata siku za mapumziko, kusikiliza changamoto zao kupitia siku maalum za "Kusikiliza Walipakodi", na kushirikiana nao ili kulipa madeni ya kodi bila kuathiri mwenendo wa biashara zao.
Mwelekeo wa Mwaka wa Fedha 2025/26
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu, mafanikio haya ni kiashiria cha matumaini makubwa kwamba lengo la mwaka mzima la ukusanyaji wa Sh. Trilioni 36.066 litafikiwa. "TRA imedhamiria kuendelea kusimamia nidhamu ya kikazi, kuimarisha mifumo ya kodi ya ndani kupitia mfumo mpya wa IDRAS, kuhimiza matumizi ya risiti za kielektroniki na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kila mlipakodi anatimiza wajibu wake.
Akizungumzia muktadha wa kisiasa, Mwenda alisisitiza kuwa TRA itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa uadilifu, uwazi na ufanisi wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ili kuhakikisha huduma muhimu za kijamii na miradi ya maendeleo zinaendelea kutekelezwa bila vikwazo.
“Kwa kushirikiana na wananchi na walipakodi wote, tunaamini makusanyo haya yatafanikishwa kwa uadilifu, uwazi na ufanisi ili kuwezesha maendeleo ya taifa letu. Pamoja tunajenga taifa letu,” amesema Mwenda
No comments:
Post a Comment