HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 10, 2025

MAFIA YAINGIA MKATABA KUKIENDELEZA KISIWA CHA TEMBONYAMA KIUTALII NA UCHUMI WA BLUU


Mwamvua Mwinyi – Mafia
Kisiwa cha Tembonyama kilichopo Kijiji cha Banja, Kata ya Kirongwe, Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, chenye ukubwa wa ekari 35, kinatarajia kuandika historia mpya kupitia uwekezaji katika sekta ya utalii.

Hatua hii inalenga kuinua uchumi wa eneo hilo na kuongeza pato la Taifa.
Kwa miaka mingi, wakazi wa kisiwa hicho wamekuwa wakitegemea shughuli za uvuvi wa mazao ya baharini ,Nazi ,Mwani na uokotaji wa tondo kama chanzo kikuu cha kipato.

Hata hivyo, mwaka 2024, kupitia Mkutano Mkuu wa kijiji cha Banja, wananchi walifikia uamuzi wa kuomba Serikali kuwatafutia mwekezaji wa kuendeleza kisiwa hicho ili kufungua fursa mpya za kiuchumi.

Ndoto hiyo sasa imetimia baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kusaini rasmi mkataba wa ukodishaji wa kisiwa hicho kwa kampuni ya Clouds Entertainment Company, kwa ajili ya uwekezaji katika masuala ya utalii.

Tukio la utiaji saini wa mkataba huo limefanyika Oktoba 9, 2025, likiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mussa Kitungi, na kushuhudiwa na Timu ya Wataalamu wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Ndugu Kitungi alieleza ,uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kutangaza utalii wa Tanzania kupitia programu ya Royal Tour.

"Kwa kutumia nguvu ileile ambayo Mhe. Rais ameitumia, na sisi katika ngazi za chini tunayaishi maono yake kwa kuhamasisha wawekezaji, tunaamini tija tuliyoikusudia tutaanza kuiona ," alifafanua Kitungi.

Nae Mwekezaji wa kisiwa hicho ,Joseph Kusaga, ambaye ni Mkurugenzi wa Clouds Entertainment, alieleza kuwa dhamira yake si kuwekeza katika utalii bali pia kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuongeza thamani ya mazao kama nazi na mwani ambayo ni miongoni mwa rasilimali za Mafia.

"Sifikirii suala la uwekezaji wa utalii pekee, tukiwa na nyinyi wataalamu tunaweza kuangalia namna ya kuongeza thamani kwa mwananchi mmoja mmoja, hasa katika zao la nazi na mwani" alieleza Kusaga.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Shabani Shabani, aliwataka wawekezaji kuona Mafia ni eneo salama na la kuvutia katika uwekezaji na ameishukuru kampuni hiyo kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuendeleza kisiwa hicho.

"Nina imani kuwa malengo yaliyowekwa yatafanikiwa, na kwa pamoja tutaona mageuzi makubwa ya kiuchumi kisiwani Mafia," alibainisha Shabani.

Kupitia hatua hii, Wilaya ya Mafia inaendelea kujiweka katika nafasi muhimu ya kukuza sekta ya utalii, kupitia uchumi wa bluu huku wakazi wake wakitarajia kunufaika kwa kupata ajira, huduma bora, na miundombinu itakayojengwa kupitia uwekezaji huo.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad