HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 10, 2025

JAMII YAASWA KUJENGA TABIA YA KUPELEKA WATOTO HARAKA VITUO VYA HUDUMA ZA AFYA KWA AJILI YA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA SARATANI.



Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Jamii imeaswa kuwapeleka watoto vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya Saratani za watoto.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu wakati akitoa elimu ya afya kuhusu Saratani za Watoto kupitia Mitandao ya Kijamii ya Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma .

Dkt. Machangu amesema ugunduzi wa mapema wa Saratani za watoto husaidia matibabu ya mapema na kuweza kupona haraka.

“Saratani za Watoto sio hukumu na kifo,ugunduzi wa mapema unasaidia kutibu tatizo hilo na nisisitize mara uonapo dalili mzazi, mlezi mchukue mtoto umpeleke katika kituo cha kutolea huduma za afya ili aweze kufanyiwa uchunguzi,matibabu ya haraka yanaweza kuchochea mtoto kupona “amesema Dkt. Machangu.

Aidha, Dkt.Machangu ameainisha baadhi ya Saratani za Watoto ni pamoja na homa za mara kwa mara, kikohozi kisichopona, kupungua uzito, kupata uvimbe, michubuko kiurahisi, kudhoofika na kuishiwa nguvu, kushindwa kutembea au kusimama vizuri, maumivu ya mifupa na viungo, upungufu wa damu,mg’ao mweupe na hata kengeza machoni, au jicho kuvimba.

“Dalili za Saratani kwa watoto zinaweza kufanana na magonjwa mengine kama homa, hivyo mtoto aonapo mojawapo ya dalili hizi usichukulie kama ni tatizo dogo ni vizuri mchukue umpeleke katika kituo cha huduma za afya”amesisitiza.

Halikadhalika, Dkt. Machangu ametaja baadhi ya aina ya Saratani zinazoweza kuwapata watoto ikiwa ni pamoja na Saratani ya Damu, Saratani ya Ubongo, Saratani ya jicho ambayo mara nyingi hugundulika kwa kuona mng’ao mweupe kwenye jicho na si kila mng’ao mweupe ni Saratani.

Ikumbukwe kuwa, Saratani za Watoto ni kundi la magonjwa ambapo inaweza kutokea pale seli za mwili zinakua na kuzaliana bila Mpangilio na tofauti kati ya saratani ya watu wazima mara nyingi saratani za watoto hazihusiani na mtindo wa maisha unaopelekea mtu kupata Saratani mfano uvutaji wa sigara, ulaji usiofaa, au tabia bwete ambapo pia saratani za Watoto hutokea kwa kasi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad