HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 10, 2025

Kundi la Afrika la Majadiliano wakutana Tanzania kujadili msimamo wa Afrika COP30



Na Mwandishi Wetu
Mkutano wa Tatu wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN) umefunguliwa Tanzania ambapo wataalamu wa Mazingira kutoka nchi 54 barani Afrika wamekutana kujadili msimamo wa Afrika kuhusu Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira ikiwa ni maandalizi kuelekea Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) utakaofanyika Brazil mwezi ujao.

Mkutano huo umefunguliwa leo Oktoba 10, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja ambaye amesema wanaendelea kufanya maandalizi ya kuwa na msimamo wa pamoja kuelekea Mkutano wa COP30 ili kuleta umoja katika Bara la Afrika.

“Lengo ni kuimarisha sauti ya pamoja ya Afrika katika utekelezaji wa Mkataba wa Paris, hasa kwenye maeneo ya fedha za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mambo mengine na Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele tangu ichukue uenyekiti wa AGN,”

“Bara letu linaendelea kukabiliwa na ukame, mafuriko na mmomonyoko wa ardhi, hivyo tunahitaji hatua za haraka na za pamoja na mkutano huu wa kimkakati unawaleta pamoja waratibu wa AGN waliokabidhiwa jukumu la kuzungumza kwa niaba ya Afrika katika ajenda mbalimbali katika mazungumzo ya kimataifa ya mazingira,” amesema Luhemeja.

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa AGN, Dkt. Richard Muyungi, amesema kikao hicho kitaimarisha mshikamano na kujenga imani mpya katika mfumo wa kimataifa wa utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi kwa haki na usawa.

“Mkutano huu pamoja na mambo mengine unaashiria wapi tulipo na wapi tunapotaka kwenda na unafanyika Tanzania kutokana na diplomasia kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anauonesha ulimwengu jinsi Tanzania ilivyokuwa kitovu cha diplomasia hasa kwenye masuala ya mabadiliko ya Tabianchi na mazingira.”

Naye, Mratibu Kiongozi masuala ya Afya na Utafiti wa AGN kutoka nchini Ghana, Dkt. Ama Essel, aliipongeza Tanzania na AGN kwa kuendelea kusukuma ajenda ya pamoja ya bara la Afrika, akisisitiza umuhimu wa fedha za mazingira kuwafikia wananchi moja kwa moja.

“Afrika inasimama kama kinara wa uvumbuzi, na fursa na mkutano huu utaangalia vipaumbele vya Afrika na mikakati ya mazungumzo katika maeneo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”

Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi si vitisho vilivyokuwa mbali bali ni hali halisi inayoishi kwa mamilioni ya Waafrika sababu mafuriko, ukame wa muda mrefu, kuongezeka kwa kina cha bahari na ukosefu wa usalama wa chakula, bara letu linabeba mzigo mkubwa wa shida ambayo haikuleta.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka Wizara za Serikali, Taasisi za Serikali na Binafsi mara baada ya kufungua Mkutano wa Tatu wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN) unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Oktoba 10, 2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua Mkutano wa Tatu wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN) unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Oktoba 10, 2025.

Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN), Dkt. Richard Muyungi akizungumza Mkutano wa Tatu wa AGN unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Oktoba 10, 2025.



Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akifungua Mkutano wa Tatu wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN) unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Oktoba 10, 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad