Pangawe, Zanzibar – 01 Oktoba 2025
MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Sera Mama ya Serikali atakayoiongoza katika Awamu ijayo itakuwa ni ajira kwa Vijana.
Akihutubia mamia ya Wanachama wa CCM na wananchi katika Uwanja wa Magirisi-Nyarugusu katika Jimbo la Pangawe ikiwa ni muendelezo wa kampeni zake za Uchaguzi Mkuu, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalifahamu kwa undani changamoto ya ajira kwa vijana na imejipanga kulitafutia suluhisho la kudumu.
Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendeleza mikakati ya kutoa ajira Serikalini, kuhamasisha ajira katika Sekta Binafsi, pamoja na kuwezesha Vijana kupata mikopo isiyo na riba kwa ajili ya kujiajiri na kuanzisha biashara zao wenyewe.
Kuhusu miundombinu, Dkt. Mwinyi amesema Serikali tayari imesaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu na barabara za ndani katika Jimbo la Pangawe na maeneo jirani kwa kiwango cha lami. Barabara ya Mambosasa–Magari ya Mchanga na barabara ya Skuli ya Kinuni–Kwarara zimetajwa miongoni mwa zitakazojengwa.
Aidha, amesema Serikali imeingia mkataba wa ujenzi wa skuli 29 za ghorofa, ambapo Jimbo la Pangawe pia litafaidika na mgao huo wa skuli za kisasa.
Kuhusu michezo, Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ijayo ina mpango wa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo katika majimbo mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya Vijana.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi amewaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar kwa Awamu nyingine na kuwapigia kura wagombea wote wa CCM katika ngazi zote, ili kufanikisha utekelezaji wa ahadi zinazotolewa kwa wananchi.
Halikadhalika, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment