Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt Amos Nungu akizungumza Septemba 30, 2025 katika Media Café iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwaajili ya kubadilishana uzoefu kati ya wanahabari na Wanasayansi.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv.
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati yake na vyombo vya habari ili kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu vinawafikia Watanzania wote.
Akizungumza Septemba 30,2025 katika Media Café, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa jamii kuhusu nafasi ya sayansi na teknolojia katika maisha ya kila siku.
“Sayansi bila mawasiliano inaweza kubaki kwenye maktaba na maabara. Ubunifu bila imani ya umma unaweza kufeli kabla haujaanza. Ndiyo maana tunataka kufanya kazi bega kwa bega na vyombo vya habari ili kila Mtanzania aone matokeo ya uwekezaji katika tafiti na ubunifu,” alisema.
Dkt Nungu akizungumzia mafanikio ya COSTECH amesema kuwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, COSTECH imefadhili zaidi ya miradi 400 ya utafiti na ubunifu yenye thamani ya shilingi bilioni 40. Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni pamoja na aina 12 za mazao yanayostahimili ukame,
Mbolea na viua wadudu hai sita pamoja na teknolojia tisa za umwagiliaji kwa kutumia nishati ya jua, zinazotumika na zaidi ya wakulima 15,000.
Ufadhili wa teknolojia zaidi ya 15 za uchakataji mazao, uliosababisha ajira kwa watu zaidi ya 200.
Kuanzishwa kwa zaidi ya vituo 50 vya ubunifu vilivyounganisha startups na kampuni ndogo 120, ambapo 60% vinaongozwa na vijana, na tayari vimezalisha ajira 2,500.
Uanzishwaji wa ofisi 45 za uhamishaji teknolojia katika vyuo vikuu 20, ambazo zimewezesha ubunifu katika sekta ya chakula na afya.
Aidha, zaidi ya wakulima wadogo 200,000 wameguswa moja kwa moja na kazi za COSTECH, jamii zimepanda miti milioni 1.2, na vifaa vya uchunguzi wa gharama nafuu kwa malaria na Kifua Kikuu (TB) vimejaribiwa katika mikoa saba.
Alieleza kuwa zaidi ya Watanzania milioni 10 tayari wamesikia habari kuhusu tafiti na ubunifu kwa msaada wa vyombo vya habari.
“Nyinyi mmeeleza teknolojia ngumu kwa lugha rahisi, mmeanzisha mijadala ya umma na kusaidia jamii kuelewa jinsi sayansi inavyoweza kuboresha maisha yao,” aliongeza Dkt. Nungu
Pia aliwaomba waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na COSTECH, akisisitiza kuwa ushindi wa taifa katika kujenga uchumi wa maarifa hautapatikana bila vyombo vya habari kusimulia kwa upana matokeo ya tafiti na ubunifu.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo juu ya Habari za Sayansi, Mratibu wa Biotechnology Society of Tanzania (BST) na Mtafiti wa Kilimo, Dkt. Emmarold Mneney, alisema teknolojia ya sayansi inazidi kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza tija ya kilimo nchini.
Alisema mbegu bora zilizoboreshwa ndio suluhisho la changamoto zinazoletwa na ongezeko la watu na kupungua kwa maeneo ya kilimo.
“Ili mkulima apate mazao ya kutosha ni muhimu kutumia mbegu zilizoboreshwa. Mbegu hizo husaidia kuongeza mavuno, kupunguza umasikini na kuimarisha usalama wa chakula,” alisema Dkt. Mneney.
Aliongeza kuwa usalama wa chakula nchini unasimamiwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa kupitia Bodi ya Tathmini ya Usalama wa Chakula, ambayo hupima na kuthibitisha ubora wa bidhaa zote kabla ya kuingia sokoni au kuwafikia walaji.
Kwa upande wa Mtafiti wa Sayansi za Kilimo kutoka Kenya, Dk. David Tarus, alisema ipo haja ya kuandaa mazingira rafiki kwa tafiti za kisayansi, huku akisisitiza mchango mkubwa wa wanahabari katika kuripoti na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa sayansi na teknolojia kwenye masula yote ya kijamii
Matukio Mbalimbali katika picha.
No comments:
Post a Comment