Ruvuma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, ameutaka Mgodi wa Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Limited kuhakikisha unaendeleza uzalishaji wake kwa kuzingatia bei za soko la sasa, ili kunufaisha mgodi wenyewe pamoja na jamii inayouzunguka.
Akizungumza Septemba 30, 2025, wakati wa ziara yake mkoani Ruvuma akiwa ameambatana na Kamati ya Ushirikishwaji ya Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Lekashingo alisema mgodi huo unapaswa kutumia mbinu za kisasa zinazopunguza gharama za uzalishaji ili kuongeza tija na faida.
Alisisitiza pia umuhimu wa mgodi kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, jambo linalosaidia kudumisha amani, usalama na ufanisi katika sekta ya madini.
Dkt. Lekashingo aliwataka viongozi wa mgodi wenye ujuzi kushirikisha na kuwafundisha wengine, ili kuongeza ushirikiano na ufanisi siyo tu ndani ya mgodi huo, bali pia katika migodi mingine nchini.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa kampuni hiyo kuhakikisha Watanzania wanapatiwa mafunzo na nafasi za ajira katika sekta ya makaa ya mawe.
Aidha, aliwataka viongozi wa mgodi kuhakikisha wanadhibiti vumbi katika maeneo ya makazi na shule jirani na mgodi, kwani hali hiyo inaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya za wananchi.
Dkt. Lekashingo pia aliwapongeza viongozi wa mgodi kwa uwajibikaji wao na kwa kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa mapana ya taifa.
“Nyie ni wadau wetu kwa sababu mmepewa kibali cha kufanya kazi hapa Tanzania. Ni jukumu letu kuhakikisha mnafanya biashara yenye faida ili muweze kulipa kodi na sisi tuweze kukusanya maduhuli,” alisema.
Ziara hiyo ilihusisha pia viongozi mbalimbali wa Tume ya Madini, wakiwemo Makamishna wa Tume, Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi, pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, CPA Venance Kasiki.
Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa Ruvuma Coal Limited Joseph Robert alimshukuru Mwenyekiti wa Tume ya Madini kwa kutembelea mgodi huo na kutoa ushauri utakaosaidia kuboresha uzalishaji na kuchangia maendeleo ya jamii inayouzunguka.
Wednesday, October 1, 2025

Home
Unlabelled
Dkt. Lekashingo Auelekeza Mgodi wa Ruvuma Coal Kuimarisha Uzalishaji
Dkt. Lekashingo Auelekeza Mgodi wa Ruvuma Coal Kuimarisha Uzalishaji
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment