Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) umetoa rai kwa vyama vya siasa na wagombea nchini kuepuka kuwatumia wanafunzi na watoto katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ukisisitiza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za watoto na kinyume cha sheria.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, wanachama wa umoja huo wamesema kumekuwepo na matukio ya wanafunzi kutolewa darasani kushiriki mikutano ya kampeni, hali ambayo ni hatari kwa usalama, ustawi na haki ya mtoto ya kupata elimu.
Mkuu wa Idara ya Utafiti, Ubunifu na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu, Bw. Makumba Mwemezi, aliyemuwakilisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, amesema ni wajibu wa asasi za kiraia kulinda watoto hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Malezi na makuzi ya mtoto ni suala la kitaifa linalovuka mipaka ya kisiasa. Tunataka kuona asasi za kiraia zikisikia na kuzungumza kwa niaba ya watoto, badala ya kunyamaza wakati haki zao zinavunjwa,” amesema Mwemezi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu kutoka shirika la My Legacy, Amina Ali, amesema kuna viashiria vya ongezeko la matumizi ya watoto kwenye shughuli za kisiasa, jambo linalokiuka Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (Tanzania Bara) na Sheria ya Mtoto Zanzibar Na. 6 ya mwaka 2011.
“Tunahimiza vyama vyote vya siasa na wagombea kujitenga kabisa na matumizi ya watoto kwenye kampeni. Ni hatari kwa makuzi yao na ni kinyume cha sheria,” amesema.
Naye Meneja Mradi kutoka Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Rogasian Masawe , ameongeza kuwa mazingira ya kampeni si rafiki kwa watoto kutokana na msongamano, kelele, lugha kali na vurugu zinazoweza kutokea.
Naye Meneja Mradi kutoka Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Rogasian Masawe , ameongeza kuwa mazingira ya kampeni si rafiki kwa watoto kutokana na msongamano, kelele, lugha kali na vurugu zinazoweza kutokea.
“Watoto hawapaswi kuwepo katika mazingira hayo, hata kama ni kama watazamaji tu,” amesema
Kwa upande wake, Bi. Cleopatra Ngesi kutoka TAMWA, ametoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha havitumii picha au kauli zinazodhalilisha watoto katika taarifa za uchaguzi.
“Ni wajibu wa wanahabari kuwalinda watoto badala ya kuwafanya nyenzo za kisiasa,” amesema.
Aidha, Mratibu wa Mradi wa Jukwaa la Utu wa Toto (CDF), Irene Ernest, amewasihi wazazi na jamii kuhakikisha watoto hawaingii maeneo ya kampeni, vituo vya kupigia kura au mikusanyiko ya kisiasa.
“Wazazi wanapaswa kuwa walinzi wa mstari wa mbele wa watoto wao. Huu si wakati wa kuwaacha mitaani au kuwapeleka kwenye mikutano ya kisiasa. Haki ya mtoto ya kulindwa ni ya kikatiba,” amesema Bi. Irene.
Kwa pamoja, wanachama wa NSSC wamesema wanatarajia kuona Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa amani huku haki na usalama wa watoto vikitangulizwa mbele kama kipaumbele cha taifa.
No comments:
Post a Comment