Na Mwandishi Wetu, Handeni.
Wanafunzi wa Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga sasa wanaondokana na adha ya kutembea kilometa 22 kila siku kufuata elimu, baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa Shule ya Amali ya Mapinduzi kupitia Mpango wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh milioni 584.2 unatajwa kuwa mkombozi kwa mamia ya wanafunzi, huku ukiwa chachu ya kuongeza ufaulu na hamasa ya masomo katika eneo hilo la Tanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, alisema kukamilika kwa shule hiyo ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha elimu bora inapatikana karibu na wananchi.
“Watoto wetu sasa hawatatembea tena mwendo mrefu. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo na tunamshukuru sana Rais Samia kwa uwekezaji huu,” alisema Ukwaju, huku akitoa maelekezo ya kupanuliwa kwa eneo la shule hiyo ili kujengewa viwanja vya michezo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Hadija Kingimali, alibainisha kuwa shule hiyo mpya ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 320. Tayari wanafunzi 53 wa kidato cha kwanza kutoka Shule ya Kwenjugo wanatarajiwa kuhamishiwa rasmi kuanza masomo Septemba 15, 2025.
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwenjugo, John Rajabu, alisoma taarifa ya ujenzi akieleza kuwa mradi huo ulianza Septemba 27, 2024, na umehusisha ujenzi wa majengo 13 ya kisasa ikiwemo maabara za baiolojia na kemia, pamoja na jengo la Tehama lenye vifaa vya kisasa.
Wakazi wa Handeni wameipongeza serikali kwa mradi huo, wakieleza kuwa utapunguza utoro wa wanafunzi, kuongeza ufaulu na kuchochea ari ya elimu hasa kwa watoto wa vijijini.





No comments:
Post a Comment