HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 11, 2025

Masai Adventure Safari na Serene Beach Resort Wafanya Usafi Fukweni, Wataka Jamii Iwajibike

 

Picha ya pamoja mara baada ya wafanyakazi wa Serene Beach Resort na Masai Adventure Safari wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2025.

TAKA za plastiki zimeelezwa kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi na uzuri wa mandhari ya Tanzania, huku wadau wa mazingira wakisisitiza kuwa suluhisho la kudumu lipo mikononi mwa jamii yenyewe.

Kampuni ya utalii ya Masai Adventure Safari kwa kushirikiana na Serene Beach Resort, leo Septemba 11, 2025, wamefanya shughuli ya usafi wa fukwe jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa jamii kushirikiana kulinda mazingira dhidi ya taka za plastiki.

Mkurugenzi wa Masai Adventure Safari, Bi. Erika Tola, alisema Tanzania ni nchi nzuri yenye mandhari ya kipekee, lakini taka za plastiki zinazotapakaa zinatishia uzuri wa asili na afya za wananchi.

“Nilipofika Tanzania niliona taka nyingi za plastiki. Ni jambo la kusikitisha kwa sababu plastiki inapoingia baharini, samaki huimeza, kisha baadaye tunapokula samaki tunakula plastiki pia. Hali hii inaleta hatari ya maradhi makubwa ikiwemo saratani,” alisema.

Ameongeza kuwa plastiki inapochomwa, moshi wake una madhara makubwa kiafya, na hivyo jamii inapaswa kushirikiana kukusanya na kuchakata plastiki ili kulinda mazingira na afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Masai Adventure Safari, Jakobo Kibori, aliwataka wananchi kuwa mabalozi wa mazingira kwa kuhakikisha plastiki inahifadhiwa vizuri na sio kutupwa ovyo.

“Mimi na wewe tuwe balozi wa mazingira. Unaponunua maji au kinywaji chochote kilichomo kwenye chupa ya plastiki, tusitupilie ovyo hata kama ni porini, kwenye fukwe au barabarani. Tuhifadhi plastiki mpaka inapochukuliwa na wahusika kwa ajili ya kuchakatwa. Kufukia plastiki fukweni si suluhisho, bali ni kuongeza tatizo,” alisema Kibori.

Aidha, Afisa Uhusiano wa Serene Beach Resort, Anna Khaday, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha elimu ya kudhibiti taka za plastiki inatolewa kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili kuongeza uelewa wa jamii.

“Sisi Serene Beach Resort tumeshaweka mikakati ya kudumu kwa kuweka vifaa vya kuhifadhia taka ngumu, hasa plastiki. Tukipewa elimu ya kutosha, itawezekana kabisa kudhibiti taka hizi ambazo ni hatari kwa afya za binadamu na kuheshimu mazingira yetu,” alisema Khaday.











Matukio mbalimbali ya wafanyakazi wa Serene Beach Resort na Masai Adventure Safari wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad