HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 11, 2025

TIRDO WATOA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI WA WILAYA YA KINONDONI

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limeendelea kutoa elimu juu ya njia bora za kuzalisha na kuhifadhi mazao ya baharini, hususan samaki na mwani.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyotolewa kwa wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji na uhifadhi wa samaki kutoka Kata ya Kunduchi katika Manispaa ya Kinondoni yamelenga kuwajengea uwezo ili waweze kufikia malengo ya kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mtaalamu wa Usindikaji Bidhaa za Chakula kutoka TIRDO, Bw. Gasper Shirima, ambaye pia ni Afisa Utafiti, alishiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ambapo alitoa salamu za Shirika la TIRDO na Kitengo cha Food Processing & Biotechnology. Aidha, aliwafahamisha washiriki huduma mbalimbali zinazotolewa na kitengo hicho kwa wajasiriamali na wenye viwanda, hasa katika kuongeza thamani ya bidhaa za chakula na mazao ya baharini.

Bw. Shirima alibainisha kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwani wajasiriamali walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo mbinu bora za ukaushaji wa samaki kwa njia ya jua, mbinu sahihi za ukataji wa samaki, na namna salama za kuhifadhi bidhaa hizo kwa matumizi ya baadaye.

Katika kuendeleza teknolojia ya viwanda nchini, TIRDO imekuwa mstari wa mbele kutoa mafunzo mbalimbali kwa wamiliki wa viwanda vikubwa, vya kati na wajasiriamali wadogo. Hadi sasa, TIRDO imetoa mafunzo kuhusu ukaushaji wa bidhaa za baharini kama samaki na mwani, pamoja na uzalishaji bora wa nishati mbadala inayotokana na mabaki ya vyakula na mimea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Chakula na Bioteknolojia, Dkt. Ivy Matoju, aliwahimiza wajasiriamali hao kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango, na pale wanapokumbana na changamoto wasisite kuwasiliana na wataalamu wa TIRDO kwa msaada. “Sisi tuna wataalamu wa sekta mbalimbali na tupo tayari kuwasaidia pale mtakapohitaji msaada wetu,” alisisitiza Dkt. Matoju.

Aidha, Dkt. Matoju alieleza kuwa katika kufanikisha mafunzo hayo, TIRDO imeshirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la VSO kutoka Uingereza, pamoja na SIDO na Suvey Fish Market.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad