HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 11, 2025

OCPD YAHIMIZA USAHIHI KWENYE UANDISHI WA HABARI ZA MASUALA YA KISHERIA NCHINI

 

 Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Jamii na Wanahabari wametakiwa kutambua kuwa Katiba inabeba masharti ya jumla ya masuala mbalimbali ya nchi lakini masharti hayo yanafafanuliwa zaidi kupitia Sheria, kanuni na Miongozo, hivyo jamii isidai yaliyoandikwa kwenye katiba moja kwa moja bila kutafuta ufafanuzi zaidi na kuhisi wananyimwa haki zao.

Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Bw. Onorius Njole wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Bw. Onorius Njole wakati akiwasilisha mada yake kuhusu uanzishwaji wa Ofisi, majukumu na mafanikio ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwenye kikao kazi kati ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kilichaondaliwa na Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

“Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya watu kuwa wananyimwa haki fulani fulani za kikatiba bila kujua kuwa Katiba inabeba sharti la jumla la jambo fulani lakini jambo hilo linafafanuliwa zaidi kwenye Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. Mfano mzuri Katiba inasema mtu ana haki ya kuishi lakini ukiingia kwenye Sheria unakutana na adhabu ya kunyongwa kwenye ukifanya mambo fulani ya jinai yaliyoaanishwa hivyo huwezi kusema unasimamia katiba na ukatenda jinai” alifafanua Bwana Njole.

Aliongeza “Mfano mwingine mzuri katiba inasema kila mtanzania ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa lakini ukisoma katiba katika eneo hilo unakutana na Sheria ya uchaguzi pengine na miongozo ya pale kwa Mkurugenzi wa uchaguzi inasema kupiga kura mwisho saa 12 jioni hivyo ukienda saa mbili usiku utakosa haki yako ya kuchagua na hutakiwi kusimama na haki ya katiba kwa kusema katiba inanipa haki ya kuchagua ninayemtaka”.

Bw. Onorius Njole amewataka Wahariri hao wa vyombo vya habari kuhakikisha wanasaidia kutoa habari, Makala na chambuzi ambazo zitasaidia jamii kuelewa mambo hayo ya kikatiba na Sheria ili kuodoa malalamiko na sintofahamu zinazojitokeza kwenye jamii kwa kutojua kile wanachokidai na katika mazingira gani.

Akieleza mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano kwenye Ofisi ya Mwansheria mkuu wa Serikali amesema sekta ya Sheria imekuwa kila mwaka kutokana na mabadiliko ya Muundo na mageuzi makubwa ya uanzishwaji wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ambayo imewezesha kukamilika kwa zoezi la Urekebu wa Sheria na kutoa toleo la Urekebu la mwaka 2023, Kufanya ufasili wa Sheria kuu 433 kati ya Sheria 446 kuwa kwenye lugha ya Kiswahili na kuwezesha jamii kupata Sheria kwa lugha mama.

Aidha, Ofisi Ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imefanya upekuzi wa mikataba ya kitaifa na kimataifa 3446 inayohusu ununuzi,ujenzi, ukarabati, kufanya upekuzi wa Hati za mashirikiano (MoU) 729, kutunga Sheria 68 huku Sheria ndogo 5,708 zimetengenezwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya maendeleo ya nchi na jamii na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo kwenye sekta mbalimbali .

Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria nchini amesema Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wa kina kwa Wahariri na waandishi wa habari kwenye kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria yaliyo chini ya ofisi yake ili kuwa na uelewa wa pamoja wa mchakato mzima wa uandishi wa Sheria nchini kwa maslahi mapana ya jamii na taifa.

Awali akifungua kikao kazi hicho Naibu Mwansheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samweli Maneno amewataka Wahariri wa vyombo vya habari na wanahabari wanapoandika habari zinazohusu masuala ya kisheria nchini kuhakikisha wanapata ufafanuzi kwa mamlaka sahihi ili kuondoa upotoshwaji ambao unaweza kuleta madhara makubwa kwa nchi na jamii.

 “Tunatambua kuwa nyinyi wahariri ndio wenye mamlaka ya mwisho ya kuamua kuhusu kutangazwa kwa kila habari ianyoonekana kwenye vyombo vyenu hivyo mna jukumu kubwa la kuhakikisha habari hizo zimetoka kwenye mamlaka sahihi hasa habari zinazohusu masuala ya kisheria, hivyo kwa kupitia kikao hiki mtaweza kuelewa watu sahihi na mamlaka ambazo zinaweza kuwasaidia kupata taarifa sahihi ili kujenga uaminifu kati yenu na walaji wa taarifa” Alisema Mhe. Maneno.

Mhe. Samweli Maneno  amesema malengo ya Ofisi hiyo ni kuhakikisha kuwa wanakuwa vinara katika utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2020 na ili lengo hilo liweze kufikiwa na jamii kufikia lengo hilo lazima nchi iwe na amani na utulivu ambao unatokana na uzingatiwaji wa utawala wa Sheria zinazowaongoza kwa kuzingatia haki na wajibu.

Amesema amani na umoja iliyopo nchini vikitoweka hakuna shughui yoyote ya kimaendeleo itakayoweza kufanyika katika jamii na hivyo kushindwa kutekeelza dira hiyo ambayo lengo lake ni kuleta ustawi wa watu na kuinua maisha ya uchumi kupitia shughuli mbalimbali.

Naibu Mwansheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samweli Maneno akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Mwansheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari.


Matukio katika picha wakati wa kikao kazi cha Viongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwandishi Mkuu wa Sheria na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.













No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad