HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 29, 2025

Fadhyl ang’ara tena mashindano ya Lina PG Tour Morogoro

 





MASHINDANO ya raundi ya nne ya kumuenzi mchezaji gofu wa timu ya taifa wanawake marehemu Lina Nkya, Lina PG Tour yametamatika kwa kishindo mkoani Morogoro huku mchezaji wa kulipwa (Pro), Fadhyl Nkya akiibuka tena na ushindi na kujinyakulia kitita cha Sh. Milioni 6.8.

Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 25, mwaka huu na kumalizika jana yameshirikisha wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro), ridhaa (Elite Amateurs) na wasindikizaji kutoka maeneo mbalimbali nchini huku Fadhyl akishinda mara tano mfululizo.

Mbali na Fadhyl mshindi wa pili kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro) ni Rajab Iddy aliyepata Sh. Milioni 4.3 huku nafasi ya tatu na nne ikichukuliwa na Hassan Kadio pamoja na Nuru Mollel, nafasi ya tano ni John Said, wa sita ni Elisante Lembris na nafasi ya saba ni John Leonce.

Kwa upande wa wachezaji wa ridhaa (Elite Amateurs), mshindi wa kwanza ni Isiaka Dunia aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 2.2, nafasi ya pili ikichukuliwa na Enoshi Wanyeche aliyepata Milioni 1.3 huku nafasi ya tatu ni Hawa Wanyeche aliyepata Sh. 900,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Nkya alisema kuwa siri ya ushindi wake wa mara tano mfululizo ni mazoezi ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyafanya.

Alisema amekuwa akisafiri nchi mbalimbali kushiriki michuano ya gofu na kwamba kabla ya kwenda huko anahakikisha anafanya mazoezi ya kutosha ili kujiweka tayari kushindana na wachezaji wengine.

“Unajua huu mchezo kila mtu anaouwezo wa kushinda, hata hivyo nimekuwa nikisafiri sana nje ya nchi kucheza michuano ya kimataifa ambayo imenifanya niwe katika kiwango kizuri kushiriki katika michuano hii ya ndani,” alisema Nkya.

Aidha alisema ili nchi iweze kupata medali mbalimbali za kimataifa katika mchezo huo wanahitaji mashindano mengi na wadau kujitokeza kwa wingi ili wachezaji waweze kupata michuano mingi ya kucheza kwa mwaka.

Naye Miongoni mwa wasimamizi wa Lina PG Tour, Enock Magile amewashukuru wachezaji wote waliojitokeza na kuwataka walewote ambao hawakufanya vizuri kuendelea na mazoezi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki mashindano yajayo.

Alisema raundi ya tano na ya mwisho ya mashindano hayo kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika Novemba na kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko itafanyika katika Viwanja vya Kili Gofu mkoani Arusha.

“Wachezaji wanaoshiriki kwa sasa ni wengi hivyo tunashukuru mashindano Morogoro yalianza vizuri na yamemalikiza kwa wakati, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, tuwaombe tu wachezaji waendelee kujiandaa na raundi ya tano ili kuhakikisha tunawapata wawakilishi wazuri katika michuano ya kimataifa,” alisema Magile

Mshindi wa jumla wa raundi ya tano ya Lina PG Tour ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai mwakani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad