HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 29, 2025

Lina PG Tour msimu wa nne wamalizika kwa kishindo Morogoro

 








MICHUANO ya raundi ya nne ya kumuenzi mlezi na mwendelezaji wa gofu ya wanawake aliyefariki dunia miaka ya hivi karibuni Lina Nkya, Lina PG Tour imetamatika kwa kishindo mkoani Morogoro huku baadhi ya wachezaji walioibuka na ushindi wakijipatia zawadi mbalimbali zikiwemo fedha.

Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 25, mwaka huu na kumalizika jana yameshirikisha wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro), ridhaa (Elite Amateurs) na wasindikizaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Katika michuano hiyo mshindi wa kwanza kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa (Mapro) ni Fadhyl Nkya aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 6.8, wa pili ni Rajab Iddy aliyepata Sh. Milioni 4.3 huku nafasi ya tatu na nne ikichukuliwa na Hassan Kadio pamoja na Nuru Mollel.

Kwa upande wa wachezaji wa ridhaa (Elite Amateurs), mshindi wa kwanza ni Isiaka Dunia aliyejinyakulia kiasi cha Sh. Milioni 2.2, nafasi ya pili ikichukuliwa na Enoshi Wanyeche aliyepata Milioni 1.3 huku nafasi ya tatu ni Hawa Wanyeche aliyepata Sh. 900,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Miongoni mwa wasimamizi wa Lina PG Tour, Enock Magile amewashukuru wachezaji wote waliojitokeza na kuwataka walewote ambao hawakufanya vizuri kuendelea na mazoezi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki mashindano yajayo.

Alisema raundi ya tano na ya mwisho ya mashindano hayo kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika Novemba na kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko itafanyika katika Viwanja vya Kili Gofu mkoani Arusha.

“Wachezaji wanaoshiriki kwa sasa ni wengi hivyo tunashukuru mashindano Morogoro yalianza vizuri na yamemalikiza kwa wakati, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, tuwaombe tu wachezaji waendelee kujiandaa na raundi ya tano ili kuhakikisha tunawapata wawakilishi wazuri katika michuano ya kimataifa,” alisema Magile

Kwa upande wake mshindi katika mashindano hayo kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa, Fadhyl Nkya amefunguka siri ya ushindi wake kwa mara tano mfululizo ni mazoezi ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyafanya.

Alisema amekuwa akisafiri nchi mbalimbali kushiriki michuano ya gofu na kwamba kabla ya kwenda huko anahakikisha anafanya mazoezi ya kutosha ili kujiweka tayari kushindana na wachezaji wengine.

“Unajua huu mchezo kila mtu anaouwezo wa kushinda, hata hivyo nimekuwa nikisafiri sana nje ya nchi kucheza michuano ya kimataifa ambayo imenifanya niwe katika kiwango kizuri kushiriki katika michuano hii ya ndani,” alisema Nkya.

Aidha alisema ili nchi iweze kupata medali mbalimbali za kimataifa katika mchezo huo wanahitaji mashindano mengi na wadau kujitokeza kwa wingi ili wachezaji waweze kupata michuano mingi ya kucheza kwa mwaka.

Mshindi wa jumla wa raundi ya tano ya Lina PG Tour ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai mwakani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad