Mwenyekiti wa Jukwaa la Watendaji Wakuu ( CEOrt Roundtable) Bw.David Tarimo akiongea wakati wa kuwapa vyeti washiriki wa kozi ya kuandaa watendaji wakuu katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Watendaji nchini ( CEOrt Roundtable) Bi Santina Benson akikabidhi tuzo kwa Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Bw. Nguvu Kamando , mmoja wa washiriki wa mafunzo ya awamu ya tano ( CAP COHORT 5 ) yaliyotolewa na CEOrt kwa Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali binafsi ili kuwapa mbinu za uongozi wenye ubunifu na maadili kwa ajili ya maendeleo ya taasisi zao na kukuza uchumi kwa ujumla.
Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Watendaji Wakuu ( CEOrt Roundtable ) Bi Santina Benson akiongea wakati wa kuwatunuku vyeti watendaji kutoka taasisi mbalimbali waliohudhuria mpango wa kuwajengea uwezo ili kuwa viongozi bora wenye weledi katika taasisi zao na kuhimiza uwajibikaji. Tukio hilo limefanyika katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro na kuhudhuliwa na watendaji mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali.

Na Mwandishi Wetu
JUKWAA la Wakurugenzi Wakuu Tanzania (CEO Roundtable - CEOrt) limepongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uongozi wa maadili na uwajibikaji nchini kupitia Mpango wa mafunzo kwa Wakurugenzi Wakuu (CEO Apprenticeship Programme - CAP), unaolenga kuwaandaa viongozi wa kizazi kijacho kushika nafasi za uongozi katika taasisi binafsi hapa nchini.
Mpango huu ulioanzishwa mwaka 2019 kwa idhini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, umelenga kuziba pengo la uongozi lililokuwepo nchini, ambapo nafasi nyingi za juu zilikuwa zikitegemea wataalamu wa kigeni. Kupitia CAP, wataalamu wa Kitanzania wenye vipaji wamekuwa wakipewa mafunzo ya kina kuhusu uongozi wa kimataifa, maadili ya kazi, na uwajibikaji kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu 20 wa kundi la tano wa mpango huo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Uongozi ( Uongozi Institute ) Balozi Ombeni Sefue ambaye pia Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu , aliisifu CEOrt kwa kuanzisha mpango huu wa kipekee unaochangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa uongozi wa nchi.
“Kinachonigusa zaidi kuhusu mpango huu ni kuwa moja ya majukumu makuu ya taasisi ninayoiongoza ni kukuza na kuandaa viongozi waadilifu na wazalendo – hasa katika sekta ya umma lakini pia sekta binafsi. Kwa hiyo, kama CAP inavyolenga kukuza viongozi wakuu wa sekta binafsi, nasi tunafanya hivyo kwa sekta ya umma. Ushirikiano wetu kupitia CAP umeendelea kuzaa matunda kwa taifa,” alisema Balozi Sefue.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CEOrt, Bw. David Tarimo, alisema jukwaa hilo linajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa viongozi bora wanaoongoza taasisi katika sekta mbalimbali kama vile fedha, teknolojia, afya na viwanda.
“Kupitia CAP, zaidi ya wahitimu 90 wamepata mafunzo ya kipekee ya uongozi. Zaidi ya asilimia 30 ya wahitimu hao tayari wameshikilia nafasi za juu za uongozi serikalini na katika sekta binafsi wakiwemo wanawake. Tunaendelea kuhakikisha kuwa kila mwaka tunakuwa na angalau asilimia 25 ya washiriki wanawake katika mpango huu,” alisema Bw. Tarimo.
Bw. David Nchimbi, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, alisema mpango huo ni jibu la changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa viongozi wa juu wenye weledi, mtazamo wa kimkakati, na uwezo wa kusimamia taasisi kwa mafanikio.
“Baadhi ya taasisi hapa nchini zimekuwa na upungufu wa viongozi wa ngazi ya juu waliokomaa kiuongozi, hivyo CAP inasaidia kujenga msingi imara wa uongozi wa ndani unaoelewa mazingira ya Tanzania na uwezo wa kushindana kimataifa,” alisema Bw. Nchimbi.
Naye Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti, Bw. Simon Shayo, alisema ukuaji wa sekta binafsi hauwezi kufikiwa bila uongozi thabiti wa maadili. Alisisitiza kuwa mafanikio ya kiuchumi yanahitaji viongozi wanaojali uadilifu na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Bi. Santina Benson, alisema malengo ya mpango wa CAP ni kuandaa viongozi wabunifu, waaminifu, na wenye maono ya kuleta mabadiliko chanya katika taasisi wanazoziwakilisha.
“Kupitia mafunzo haya, CAP inajenga kizazi kipya cha viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko,” alisema Bi. Santina.
Wahitimu wa mpango huo pia walielezea namna walivyonufaika. Nguvu Kamando, Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom, alisema CAP ni chombo madhubuti kilichomsaidia kukuza uwezo wake wa uongozi kwa kupitia mafunzo ya kina yanayotolewa na wakufunzi wabobezi.
Naye Bi. Anitha Raymos, Meneja Mkuu wa Silent Ocean, alisema mafunzo aliyopata yamemsaidia kujua kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza kwa umahiri sawa na wanaume, na kusisitiza kuwa uongozi wa kijinsia haupaswi kuwa na mipaka.
Katika hafla hiyo, taasisi na wadau waliotoa mchango mkubwa katika ufanikishaji wa mpango huo walitunukiwa tuzo za heshima. Miongoni mwa waliotunukiwa ni pamoja na kampuni ya Derm Group, Bakhresa Group, benki za CRDB na NMB, pamoja na Bw. Carl Wagner wa Strathmore Global na Bw. Roger Boniface wa Edisim.
Mpango wa CAP umebuniwa ili kujenga daraja kati ya kizazi cha sasa cha viongozi watarajiwa katika taasisi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment