Na Emmanuel Massaka – Michizi TV
Serikali imezindua rasmi Bodi mpya ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi katika sekta ya utumishi wa umma nchini. Uzinduzi huo umefanyika katika kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao cha chuo hicho.
.jpeg)
Bw. Mkomi aliwapongeza wajumbe wapya wa bodi na kueleza kuwa uteuzi wao umezingatia weledi, uadilifu na uzoefu katika nyanja mbalimbali. Alibainisha kuwa jukumu kuu la bodi ni kuhakikisha chuo kinatoa mafunzo yanayoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa, pamoja na kutoa mchango katika mageuzi ya sekta ya umma.
Amesisitiza kuwa wajumbe wa bodi wanapaswa kutoa dira na ushauri wa kimkakati utakaowezesha chuo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kusimamia rasilimali kwa ufanisi, na kuimarisha nidhamu na maadili katika utumishi wa umma. Aidha, serikali imeahidi kuendelea kutoa mwongozo na sera zitakazowezesha chuo kutimiza malengo yake.
Wakati wa hafla hiyo, Bw. Mkomi aliwatambulisha wajumbe wa bodi wapya wakiongozwa na Dkt. Florens Martin Turuka (Mwenyekiti), Dkt. Ernest Francis Mabonesho (Katibu), pamoja na wajumbe wengine: Mhe. Jaji (Mstaafu) Awadh Mohamed Bawazir, Prof. Masoud Hadi Muruke, Balozi John Ulanga, Dkt. Faraja Teddy Igira na Bi. Leila Maurilyo Mavika.
Akitoa taarifa ya utendaji wa bodi iliyomaliza muda wake, Dkt. Florens Turuka alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, chuo kilipata hati safi za ukaguzi wa serikali mfululizo, jambo alilolieleza kuwa ni alama ya uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha. Aliongeza kuwa bodi iliidhinisha sera na mifumo kadhaa ya kitaasisi ikiwemo sera za utafiti, TEHAMA, ubora wa huduma na miundombinu.
Katika kipindi hicho, jumla ya wanachuo 43,753 walihitimu, na zaidi ya watumishi 46,000 wa umma walipatiwa mafunzo ya muda mfupi. Pia tafiti tumizi nane na machapisho 43 yaliandaliwa na chuo, huku zaidi ya watumishi 4,000 wakifaulu mitihani ya utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, alisema kuwa zaidi ya watumishi 47,000 wa umma wamepatiwa mafunzo katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na bodi iliyotangulia. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yaligawanywa katika makundi ya umahiri, uongozi, maadili, utawala bora, na ujenzi wa uwezo.
Aidha, Dkt. Mabonesho alibainisha kuwa miradi ya miundombinu inaendelea kuimarishwa, ikiwemo kukamilika kwa awamu ya pili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida kwa gharama ya Sh bilioni 2.2, na hatua nzuri za ujenzi wa Kampasi ya Tanga kwa ufadhili wa serikali. Pia alieleza kuwa chuo kina jumla ya watumishi 372, na kimeendelea na mikakati ya kuajiri, kuendeleza na kuwapandisha vyeo watumishi wake.
No comments:
Post a Comment