Akizungumza wakati wa maonesho hayo Bw. Peter Namaumbo, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi amesema TBS imefika katika maonesho haya kutoa elimu ya uelewa wa masuala matakwa ya viwango kwa wazalishaji wa bidhaa na watumiaji wa bidhaa hizo
Bw. Namaumbo amesema kuwa elimu hii imetolewa kwa wajasiriamali walioshiriki maonesho haya ambapo TBS imewatembelea katika mabanda yao kuwaeleza taratibu za kupata alama ya ubora kwa wale ambao hawakuwa na elimu hiyo lakini pia kuzungumza nao na kujua changamoto wanazozipitia zinazowakwamisha kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TBS inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali wadogo na wa kati bila gharama yoyote, mjasiriamali atahitajika kuanzia SIDO ambapo ataandikiwa barua inayomtambulisha kama mjasiriamali mdogo au wa kati na baada ya kupata barua hiyo basi atahudumiwa na TBS bure kabisa kwa muda wa miaka mitatu.
“Tunatoa wito kwa wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuongeza wigo wa masoko yao ndani na nje ya nchi Kwani huduma ya uthibitishaji hutolewa bure na TBS mjasiriamali anatakiwa kuanzia SIDO tu ili kupata barua ya utambulisho basi”
Aidha ameongeza kuwa TBS imetoa elimu kwa wananchi kuwakumbusha kutotumia bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwani bidhaa hizo zinamadhara makubwa sana kiafya kitu ambacho kisipozingatiwa kinaweza kupelekea Taifa kupoteza nguvu kazi.
“Tunawakumbusha wananchi hasa dada, mama zetu na watoto wetu kutotumia vipodozi vilivyopigwa marufuku kwani bidhaa hizi zina viambata sumu vyenye madhara makubwa sana katika afya za watumiaji kwani hupelekea kansa ya ngozi, vizazi na wakati mwingine mvurugiko wa homoni, madhara yote haya mengine hupelekea kifo na mengine hupelekea kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa”
Bw. Peter amesema kuwa maonesho haya yamekuwa fursa kubwa ya kutoa elimu hii sababu vipodozi vingi vilivyopigwa marufuku vinaingia nchini kupitia njia za panya kutoka nchi jirani zinazopakana na mikoa inayopatikana katika Kanda ya Nyada za Juu Kusini.
Amesisitiza kuwa elimu hii inalenga kuwafanya wananchi kuelewa madhara ya bidhaa hizo na hatimaye kuacha kabisa kutumia bidhaa hizo na kama uhitaji wa bidhaa hizo utaisha basi hata soko la bidhaa hizo litaisha kabisa.
TBS inatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wananunua bidhaa zilizokidhi matakwa ya Viwango ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kwa kutumia bidhaa hafifu.







No comments:
Post a Comment