Njokii Kariuki kutoka taasisi ya Global Peace Initiative Nairobi, Kenya akizungumza na waandishi wa habari.
KADIRI Tanzania inavyokaribia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, waandishi wa habari wametakiwa kuwa makini na namna wanavyoripoti taarifa, hasa katika zama hizi za teknolojia ya akili bandia (AI), ambazo zimeongeza kasi ya kusambaa kwa taarifa za uongo, chuki na uchochezi mitandaoni.
Katika warsha ya siku mbili iliyofanyika mwishoni mwa wiki (Julai 17, 18, 2025) iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na mpango wa #defyhatenow kupitia Global Action for Peacebuilding (GAPI) na kwa ufadhili wa GIZ, waandishi wa habari walipewa mbinu mbalimbali za kutambua na kuepuka kusambaza habari zinazoweza kuathiri amani na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Njokii Kariuki kutoka taasisi ya Global Peace Initiative Nairobi, Kenya, alisema kuwa zipo taarifa ambazo hutengenezwa kwa makusudi ili kushawishi hisia za watu au kuharibu sifa za watu au taasisi, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
“Kuna maneno yanaandikwa kwa makusudi ya kuleta taharuki au kuchochea hisia za chuki. Waandishi wanapaswa kuwa waangalifu, kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchapisha taarifa yoyote, lazima waulize, nani alisema? Lini? Kwa muktadha upi? Na kwa lengo gani?” alisisitiza Kariuki.
Aliongeza kuwa baadhi ya taarifa hutolewa kwa kutumia muktadha wa zamani, lakini huwasilishwa kama matukio ya sasa, jambo ambalo huchangia kupotosha umma na kuibua migawanyiko ya kijamii.
Silvia Daulinge kutoka TAMWA akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Silvia Daulinge kutoka TAMWA aliongeza kuwa waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ulimwengu wa kidijitali ambapo taarifa zisizo sahihi husambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo rasmi vya habari.
“Kumekuwa na ongezeko la hotuba za chuki na udhalilishaji hasa dhidi ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi. Wanawake, vijana na makundi maalumu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi bila kuonewa au kudhalilishwa,” alisema.
Silvia alisisitiza kuwa mitandao ya kijamii imetoa fursa kwa kila mtu kutoa maoni, lakini jukumu la waandishi wa habari ni kuchambua kwa makini taarifa hizo na kuziwasilisha kwa jamii kwa njia inayojenga na si kubomoa.
“Teknolojia ya akili unde (AI) imerahisisha utengenezaji wa picha bandia, sauti na hata video zinazoweza kuaminika kuwa halisi. Waandishi wanahitaji maarifa mapya ya kutambua uhalisia wa taarifa kabla ya kuzitangaza,” aliongeza.
Kwa Upande wa Florence Majani kutoka TAMWA alisisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si tatizo, kwa kutumia kalamu zao kujenga jamii yenye mshikamano na kulinda misingi ya haki, usawa na demokrasia.
“Katika kipindi hiki, tunawashauri waandishi kutumia misingi ya maadili ya uandishi wa habari, kuhakikisha sauti za makundi yote – wanawake, vijana, watu wenye ulemavu – zinasikika bila woga na kwa heshima. Tusitumie majukwaa yetu kueneza kauli zinazochochea au zinazodhalilisha utu wa mtu,” alihitimisha.
Warsha hiyo iliwakutanisha waandishi wa habari mbalimbali nchini na kuwaletea mafunzo juu ya fact-checking, usalama wa habari mitandaoni, matumizi salama ya AI, na mbinu za kuandika taarifa zinazojenga amani wakati wa uchaguzi.
Warsha hii imekuja wakati muhimu ambapo vyombo vya habari vinatarajiwa kuwa nguzo ya amani na demokrasia, kwa kuhakikisha jamii inapokea taarifa sahihi, za haki na zisizoegemea upande wowote, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
.jpeg)
Baadhi ya waandishi wa Habari wakiwa katika mafunzo.
No comments:
Post a Comment