HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 20, 2025

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada awasili nchini kwa ziara ya Kikazi

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Randeep Sarai amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku Tatu.

Mhe. Sarai anatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Canada katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, na Zanzibar.

Miradi itakayotembelewa ni pamoja na Kituo cha Afya Makuburi na Kampuni ya Nishati Mbadala ya JAZA (Dar es Salaam); Mradi wa Kurina Asali wa Central Park Bees na Kiwanda cha kuzalisha na kusambaza unga wa Sembe-Chamwino; mkutano CRDB tawi la Dodoma pamoja na ziara katika Kituo cha Afya cha Makole, Dodoma.

Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Mhe. Sarai alipokelewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Said Shaib Mussa na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wala Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme na Balozi wa Canada nchini Mhe. Emily Burns.

Akizungumza baada ya mapokezi hayo uwanjani hapo, Mhe. Mhagama ameishukuru Serikali ya Canada kwa mchango wake wa zaidi ya Shilingi Bilioni 120 kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya nchini kupitia miradi mbalimbali.

Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Accelerated Hope and Development for Adolescents in Tanzania (AHADI), unaotekelezwa na Shirika la World Vision (Shilingi bilioni 38.8), Mradi wa Girls’ Reproductive Health, Rights and Empowerment Accelerated in Tanzania (GRREAT), unaosimamiwa na UNICEF (Shilingi bilioni 51.7), na Mradi wa Strengthening Midwifery in Tanzania, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya AMREF na Chama cha Wakunga cha Canada na Tanzania (Shilingi bilioni 30.4).

“Msaada huu wa Serikali ya Canada umesaidia Tanzania kuboresha utoaji huduma za afya kwa wananchi na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 67 kwa 1,000 mwaka 2015 hadi 43 mwaka 2022, na vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000” alifafanua Mhe. Mhagama.

Waziri huyo wa Afya ameweka bayana dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo na Canada, chini ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lengo likiwa kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa jamii, kutoa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Tanzania na Canada, pamoja na kuendeleza mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya vifo vya watoto wachanga nchini.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Randeep Sarai amesisitiza dhamira ya Canada kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania ili kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili kwa manufaa ya wananchi wake.

Ameeleza kuwa Canada itaendeleza ushirikiano wake na Tanzania katika sekta za afya, elimu, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa vijana, udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi, na misaada ya kibinadamu. Ushirikiano huu pia unatoa kipaumbele katika kuwawezesha wanawake na wasichana, kuimarisha utawala jumuishi, ujenzi wa amani, pamoja na kukuza maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla.











No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad