HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 25, 2025

Naibu Waziri Londo Aishukuru Uswisi kwa kuboresha Maendeleo ya Jamii nchini

 


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.), ameishukuru Serikali ya Shirikisho la Uswisi kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii kupitia utekelezaji wa miradi ya kisekta inayofadhiliwa na nchi hiyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Londo amesema hayo tarehe 24 Juali, 2025 katika maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Uswisi yaliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Taifa hilo hapa nchini, jijini Dar Es Salaam.

Amesema historia ya uhusiano wa Tanzania na Uswisi ilianzia mwaka 1927 wakati ilipofungua konseli yake mjini Tanga, katika hatua zake za mwanzo za ushirikiano na Tanzania, na kuwezesha ushirikiano huo kuimarika zaidi miaka ya 1960, kupitia ufadhili wa miradi katika sekta mbalimbali.

“Tunatambua Uswisi imechangia maendeleo yetu katika sekta za afya, elimu, ajira kwa vijana, kuwawezesha wanawake na makundi maalum, pamoja na sekta ya kilimo. Ufadhili huu umechangia kuboresha maisha ya wananchi na kuwezesha kufikia malengo ya maendeleo endelevu,"Alifafanua Mhe. Londo.

Aidha, aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano huo wa kirafiki kwa kuhakikisha kuwa misaada inayotolewa inaleta tija kwa wananchi na kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Uswisi, Mhe. Nicole Providoli, amesema kuwa Serikali ya nchi yake kupitia Chemba ya Biashara ya Uswisi na Tanzania (Swiss-Tanzania Chamber of Commerce - STCC), itaendelea kusaidia jitihada za pande zote mbili katika kuanzisha fursa za biashara na uwekezaji, kwa lengo la kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad