Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) imetumia Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutangaza fursa lukuki zilizopo kwenye sekta ya mkonge, huku ikitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia kilimo hicho chenye tija na soko la uhakika kimataifa.
Akizungumza katika banda la Bodi hiyo, Mkuu wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji, David Maghali alisema uwepo wao kwenye maonesho hayo ni kwa ajili ya kuwaelimisha wadau kuhusu fursa za kilimo na biashara ya mkonge, sambamba na kuhamasisha ushiriki mpana zaidi wa Watanzania katika sekta hiyo.
“Tunatoa elimu juu ya uzalishaji bora wa mkonge ili kuhakikisha kinachozalishwa kinakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Lengo letu ni kuona wakulima wanazalisha bidhaa zenye ubora ambazo zinanunulika moja kwa moja sokoni,” alisema Maghali
Alibainisha kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi bora kwa kilimo cha mkonge, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuitumia fursa hiyo kwa kuwekeza kwenye kilimo hicho ambacho hakina changamoto nyingi na kina soko la uhakika duniani.
Magale aliongeza kuwa fursa nyingine ni katika uzalishaji wa mbegu za mkonge, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya miche miongoni mwa wakulima. “Hii ni nafasi ya Watanzania kuanza kuzalisha mbegu kwa ajili ya biashara,” alisema.
Aidha, alitaja uanzishaji wa vituo vya uchakataji kuwa ni fursa muhimu, akisema kwa sasa mkonge hauuziwi kama majani bali kwa mfumo wa nyuzi, hivyo ni muhimu kwa wawekezaji kuwekeza kwenye mashine za kuchakata mkonge ili kuongeza thamani ya zao hilo.
“Kitu kikubwa tunachokifanya sasa ni kuhakikisha uzalishaji unalingana na mahitaji ya soko. Tuna kituo cha atamizi Tanga kinachotoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge kama mikoba, mikeka na bidhaa za ufumaji,” alifafanua.
Kwa upande wake, Emmanuel Lutego, Afisa Udhibiti Ubora alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika uchakataji wa mkonge ili kuongeza tija na kufikia lengo la taifa la kuzalisha zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka.
“Changamoto kubwa iliyokuwepo hapo awali ilikuwa ni upatikanaji wa miche. Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka uliopita ilisambaza zaidi ya miche milioni 2 kwa wakulima, na sasa tatizo lililopo ni uhaba wa mashine za kuchakata mkonge,” alisema Lutego.
Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kusambaza mashine 10 za uchakataji katika maeneo mbalimbali ili kupunguza changamoto hiyo na kuongeza uzalishaji wa mkonge bora, unaokubalika katika soko la dunia.
Mbali na nyuzi, Lutego alibainisha kuwa mabaki ya mkonge hutumika pia kuzalisha bidhaa nyingine zikiwemo mbolea, chakula cha mifugo, uyoga, na nzi chuma, hivyo kuongeza thamani ya zao hilo kwa namna nyingi.
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha mkonge bora duniani, na juhudi za Bodi ya Mkonge ni kuhakikisha sifa hiyo inalindwa na kuendelezwa kwa kutumia teknolojia na kuzingatia viwango vya ubora.
No comments:
Post a Comment